Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde akimkabidhi jezi Katibu Mkuu wa chama cha mpira mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) wakati kampuni ilipokabidhi vifaa vya michezo kwa timu za shule za sekondari zitakazoshiriki michuano ya Airtel Rising Stars ambayo inatarajiwa kuanza Jumatano. Hafla hiyo ilifanyika kwenye ofisi za TFF, Mei 28, 2012.
******************
Airtel Tanzania leo imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu za shule za sekondari 24 zitakazoshiriki kwenye michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 maarufu kama Airtel Rising Stars ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Jumatano, Mei 30, ngazi ya Mkoa.
Shule zitakazoshiriki kwenye michuano hiyo ni zile zilizofanya vyema kwenye michuano ya shule za sekondari (UMISSETA), ambazo ni Lindi sekondari, Mpunyule na Nkowe zote za Mkoa wa Lindi, Southern Highland, Mbeya Day na Wenda Sekondari kutoka Mbeya.
Nyingine ni Mbande Sekondari, Kurasini na Kiravi (Temeke), Airwing, Benjamini Mkapa na Msogola Sekondari (Ilala), Twiga Sekondari, Goba na Makongo Sekondari (Kinondoni), Sinoni, Kaloleni na Bishop Durning (Arusha).
Timu hizo zote zimethibitisha ushiriki wao na kuahidi kufanya vizuri ili kushinda mechi zao. Mechi za mikoa zitatumika kuchangua timu kombaini zitakazowakilisha mikoa kwenye mashindano ya Airtel Rising Stars ngazi ya taifa yatakayoanza Juni 9 mpaka Juni 17 Jijini Dar es Salaam.
Wakati timu za wavulana zikatarajiwa kushindana kwenye ngazi ya mkoa ili kuchanguliwa kucheza michuano ya Taifa, timu moja kutoka kila Mkoa itafuzu moja kwa moja na kufanya timu zitakazoshiriki ngazi ya taifa kuwa 12, sita za wavulana na sita wasichana.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, Meneja Masoko na Matangazo Airtel Tanzania Rahma Mwapachu alisema Airtel inajivunia ushirika wake na moja ya Klabu kubwa duniani - Machester United, kuinua kiwango cha mpira wa miguu nchini Tanzania na Afrika. 'Tunaamini ya kuwa kwa ushirikiano wetu na Manchester United na TFF tutakuza kwa kiasi kikubwa kiwango cha mpira wa miguu hapa nchini Tanzania. Tunaamini vijana wakiandaliwa vizuri wanaweza'.
Mwapachu alishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamanduni na Michezo kwa ushirikiano wanaotoa ili kukuza mpira hapa nchini.
Airtel Rising Stars ni mpango kabambe wa Afrika nzima ambao ni kuibua na kukuza vipaji vya wanasoka wanaochipukia, wavulana na wasichana wenye umri wa miaka chini ya kumi na saba ambao watapata muda muafaka wa kuonyesha vipaji vyao na kukutana na waatalum wa mpira wa miguu na kupata mafunzo zaidi hivyo kukuza vipaji vyao.
Mwaka jana, Klabu ya Manchester United ilitoa walimu wake wa soka la vijana kufundisha kliniki za soka za kimataifa zilizofanyika Tanzania, Afrika Kusini na Gabon ambapo walishiriki walipata nafasi ya kufundisha jinsi ya kucheza mpira wa miguu kwa mtindo wa Manchester United.
Kliniki ya aina hiyo itafanyika Jijini Nairobi Agosti mwaka huu kwa nchi zinazozungumza Kingereza Tanzania ikiwemo. Nairobi pia itakuwa mwenyeji wa mashindano ya Airtel Rising Stars inter-continental ambayo itashirikisha nchi 14 ambapo Airtel inafanya biashara. Tanzania itawakilishwa na mshindi wa fainali za taifa pamoja na wachezaji sita bora, watatu wavulana na watatu wasichana.
|
No comments:
Post a Comment