Tangazo

May 14, 2012

Mama Kikwete awataka wanawake kutotupa watoto

Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete akiangalia bidhaa za vikapu zinazotengenezwa na Mbeya Bamboo Women Group huku Bi Furaha Mwinami, mmoja wa wanakikundi hao akimweleza Mama Kikwete namna wafanyavyo kazi zao.PICHA/JOHN LUKUWI
*****************
Na Anna Nkinda – Maelezo, Mbeya

Wanawake nchini wametakiwa kutokuwatupa watoto wanaowazaa hata kama wanakabiliwa na changamoto za kimaishaza za kushindwa  kuwalea kwani kwa kufanya hivyo  wanamkosea Mwenyezi Mungu pia hawawezi jua watoto hao watakuwa na hali gani ya kimaisha kwa siku za baadaye.

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanawake waliohudhulia  sherehe za  siku ya mwanamke wa Chuo Kikuu Cha Teofilo Kisanji (TEKU) kilichopo jijini Mbeya.

Aidha  Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)  alisema  kuwa usawa wa kijinsia katika elimu na fursa za kiuchumi zimeendelea kuwa changamoto kwa  wanawake Duniani kote hata hivyo hatua kubwa imefikiwa ya  kuwakomboa wanawake wengi kutoka lindi la umasikini.

“Tunatambua kwamba wanawake wanaposhiriki kikamilifu katika shughuli za jamii uchumi wa nchi hukua zaidi. Hivyo siku kama ya leo ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha wanawake kujifunza kutoka kwa wengine jinsi walivyofanikiwa , kubadilishana uzoefu na kuelimishana. Kwani elimu yenye manufaa ni ile inayolenga kuwakomboa watu kutokana na changamoto zinazowakabili”, alisema Mama Kikwete.

Mama Kikwete aliwaasa wanafunzi wa chuo hicho kusimama imara na kuwa na mipango na malengo ya maisha baada ya kumaliza chuo, wakabiliane na changamoto  zinazowakabili, wasidanganywe na vitu vidogodogo ambavyo vinaweza kuwaharibia maisha yao ya baadaye.

Akisoma risala ya chuo Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Tuli Kassimoto alisema kuwa chuo hicho kinachomilikiwa na kanisa la  Moravian  Tanzania kilianzishwa mwaka 2006  kinajumla ya wanafunzi 3978  kati ya hao 2463 ni wanaume na 1515 ni wanawake.

Alisema kuwa tatizo kubwa linalokikabili chuo hicho ni ukosefu wa mahali pa kulala kwa wanafunzi  licha ya kuwa na idadi kubwa ya wanachuo, wanachuo 200 ndiyo wameweza kupata nafasi ya kulala chuoni wengine wanalala nje ya chuo na baadhi ya nyumba wanazolala si nzuri na hazina ubora na usalama. 

Profesa Kassimoto alisema, “Ili kutatua tatizo hili chuo kiliomba mkopo kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania walitupatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli ya wasichana ambayo itakapokamilika itachukua watu 316 hii ni idadi ndogo ukilinganisha na mahitaji”.

Alisema kuwa kwa kuzingatia matatizo yanayowakabili wanachuo wanawake, waliona umuhimu wa kuwa na siku ya mwanamke wa TEKU ambayo ilitumika kukaa pamoja kama jamii, kufurahi, kuelimishana kwa njia mbalimbali  na kuithamini nafasi ya mwanamke katika jamii.

Sherehe hiyo ilienda sambamba na uchangiaji wa fedha za mfuko wa elimu wa wanawake wa TEKU ambapo familia ya Rais Kikwete alichangia shilingi milioni tano, Taasisi ya WAMA milioni mbili pamoja na wadau mbalimbali walichangia na hivyo  kufanya fedha zilizopatikana kufikia milioni 15.

Fedha hizo zitatumika kununua vifaa vya hosteli inayojengwa na chuo hicho kwa ajili ya wanachuo wanawake na kutatua matatizo ya wanachuo wa kike.

No comments: