Tangazo

May 4, 2012

Mama Salma Kikwete aitaka Taifa Queens kuiletea Nchi Ushindi

Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wachezaji wa timu ya Netiboli ya Taifa (Taifa Queens) kufanya vizuri na kuiletea nchi  heshima katika mashindano  ya kombe la Afrika yanayotarajiwa  kuanza  jumanne ijayo jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni mlezi wa timu hiyo ameyasema hayo leo wakati akiongea na wachezaji hao alipowatembelea katika kambi yao iliyoko shule ya Filberth Bayi Kibaha  mkoani Pwani.

“Muende kwenye mashindano mkitegemea kupata ushindi na siyo kuwa wasindikizaji jambo la muhimu ni kufuata maelekezo mnayopewa na walimu wenu  na kutokutoa pasi nyuma pale unapokuwa  kwenye eneo la hatari (golini) kwa kufanya hivyo unaweza ukapoteza mpira na kumpatia adui”, alisema Mama Kikwete.

Aidha Mama Kikwete aliwaomba watanzania kuendelea kuichangia timu hiyo ili iweze kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuweza kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Kwa upande wake Meneja wa timu Deborah Mnzava alisema kuwa kambi hiyo yenye wachezaji 16 na viongozi sita imejiandaa vya kutosha ili kuweza kushiriki katika mashindano hayo licha ya kukabiliwa na upungufu wa vifaa vya mazoezi kwa hadhi ya timu ya taifa.

Akisoma taarifa ya Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) Mwenyekiti wa chama hiyo Anna Bayi alisema kuwa timu hiyo imeipatia sifa Tanzania katika medani ya kimataifa kwani kwasasa inashikilia  nafasi ya 20 katika Dunia.

Alisema kuwa chama hicho kimepewa heshima ya kuandaa mashindano ya  kombe la Afrika yanayotarajiwa kuanza tarehe 08-12/5/2012 yatakayozishirikisha nchi za Malawi, Zambia, Zimbabwe, Lesotho, Namibia, Botswana, Uganda na mwenyeji Tanzania abayo ndiyo mwenyeji.

Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo Mwenyekiti wake ni Mama Kikwete  ilitoa shilingi  milioni 10 fedha ambazo zitatumika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili timu hi
yo.

No comments: