Tangazo

May 11, 2012

TASWA yaomboleza Kifo cha Mhariri wa Michezo wa Gazeti la Mtanzania, Rachel Mwiligwa

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinaungana na familia na wanahabari wote nchini kuomboleza kifo cha Mhariri wa Habari za Michezo wa gazeti la Mtanzania Rachel Mwiligwa (Pichani).

TASWA imeshtushwa taarifa za kifo cha Rachel kilichotokea usiku wa kuamkia leo, hivyo tunatoa pole kwa familia yake, waandishi wa habari za michezo na wafanyakazi wenzake wote, wasanii na wanamichezo wengine katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mdau mkubwa wa michezo na burudani.

Kutokana na msiba huo, chama kinaandaa taratibu zake za kuwasilisha rambirambi kwa namna tulivyojiwekea, kwani marehemu hadi mauti yanamkuta alikuwa mwanachama mtiifu wa TASWA. Hivyo upo utaratibu kama mwenzetu akitangulia mbele ya haki namna gani tunatakiwa tufanye.

Lakini pia upo utaratibu mwingine nje ya chama ambao utahusu mtu binafsi kuwasilisha michango ya rambirambi, ambapo TASWA inawasiliana na wahariri wote wa habari za michezo wasaidie kukusanya michango ya rambirambi kwenye vyombo vyao, ambayo wataiwasilisha kwa wajumbe wa Kamati Maalum ya kusimamia jambo hili.

Wajumbe hao ni Angela Msangi  ambaye atakuwa Mratibu akisaidiwa na Mwani Nyangasa, ambao watashirikiana na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, George John ambaye ni Katibu Msaidizi wa TASWA, Grace Hoka na Alfred Lucas ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Tunaomba ushirikiano wa wadau katika kufanikisha jambo hili.

Msiba kwa sasa kwa mujibu wa taarifa za awali upo Manzese Tiptop,tutaendelea kujulishana kadri zitakavyopatikana taarifa mpya.

Tunaomba waandishi wa habari za michezo, wasanii na wanamichezo kwa ujumla tumuenzi Rachel kwa masuala mbalimbali aliyokuwa akiyatilia mkazo ikiwemo kusimamia ukweli kwa kile alichokiamini na ndio maana tunasema tutaendelea kumkumbuka daima. Mungu amuweke mahali pema peponi. Amin

Imetolewa na:
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
11/05/2012    


Daily Mitikasi Blog inatoa pole kwa familia ya marehemu na wanahabari wote kwa msiba huu mzito, Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu.
 
Sote tulimpenda Dada Rachel lakini Mungu amempenda Zaidi, jina la bwana lihimidiwe... AMENI

No comments: