Tangazo

May 2, 2012

Uhuru wa Vyombo vya Habari Huimarisha Jamii

Dana L. Banks
Na Dana L. Banks
 
Habari au taarifa ni nguvu. Ni watu wachache sana wanaoweza kuishi, kuiwajibisha serikali yao na kuwaelimisha watoto wao bila kuwepo kwa mtiririko huru na thabiti wa habari. 

Raia wanahitaji taarifa sahihi na zenye kuaminika, katika wakati sahihi. Vivyo hivyo kwa wafanyabiashara, masoko na hata serikali.

Watumiaji wa leo wa taarifa duniani kote wanataka kupata tarifa wanazozihitaji katika sekunde kadhaa na wala si saa au siku kadhaa. 

Kupanuka kwa njia mbalimbali za kijamii za kusambaza habari hasa kwa kupitia teknolojia ya kisasa miongoni mwa watu na hata vyombo vya habari vyenyewe, kunaashiria hamu kubwa ya umma kupata taarifa wakati wote. 

Jambo hili limekuwa kama sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Watu wengi hawawezi kuendesha shughuli zao za kila siku za kujikimu, kuwajibisha serikali zao au kuelimisha watoto wao bila kuwa mtiririko huru na thabiti wa habari. Raia wanahitaji taarifa sahihi na zenye kuaminika kwa wakati sahihi. 

Uhuru wa vyombo vya habari huzifanya jamii pamoja na uchumi wake kuchangamka, kuimarika na kustawi. Pale ambapo mtiririko huru wa habari umekatwa basi watu mmoja mmoja, jamii na hata uchumi huathirika vibaya.

Karne ya 21 imeleta mapinduzi makubwa ya mawasiliano na upashanaji habari. Mataifa na watu ambao hapo awali walikuwa wametenganishwa na mipaka ya nchi zao, wanaunganishwa moja kwa moja kwa kupitia mtandao wa mawasiliano wa Internet. 

Aidha, ni wao ndio wanaoandika na kuueleza ulimwengu mzima kuhusu hali zao. Kama tulivyoona katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jamii ambazo zinakandamiza waandishi na vyombo vya habari, haziwezi tena kufanya hivyo kwa muda mrefu kabla ya raia hawajaweza kusambaza taarifa zao na kujenga mitandao mikubwa ya upashanaji habari kwa kutumia njia za kisasa na thabiti za upashanaji habari kwa kupitia mtandao (social media tools).   

Mtandao wa Internet umepanua majadiliano na ubadilishanaji mawazo baina ya watu wa mataifa yote duniani. Kwa kiwango kikubwa mtandao huu wa mawasiliano ulichangia kuangushwa kwa tawala kandamizi Kaskazini mwa Afrika mwaka jana na ndio unawezesha raia katika nchi za Magharibi- ikiwemo Marekani - kufuatilia utendaji wa serikali zao. 

Uhuru wa vyombo vya habari umejumuishwa katika Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la Mwaka 1948 linaloeleza kuwa "Kila mtu ana haki ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni yake; haki hii inajumuisha uhuru wa kuwa na maoni bila kuingiliwa na kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa na maoni kwa kupitia njia yoyote ya upashaji habari bila kujali mipaka ya nchi."

Uongozi katika vyombo vya habari, iwe ni vile vya uchapishaji, utangazaji, mtandao wa internet na mitandao ya kijamii ni muhimu katika maendeleo ya uhuru wa habari. Hasa katika kuvifanya vyombo hivi kutokuwa vyombo vya kuisemea serikali bali vyombo huru vya ufuatiliaji. 

Uongozi ndiyo unaotoa dira na misingi ya kimaadili kwa uandishi wa habari na hivyo kujenga imani ya umma kwa vyombo hivyo. Viongozi katika tasnia ya habari Tanzania ni wale wote wanaowafundisha, kuwaongoza na kuwatia moyo waandishi wa habari wa kizazi kijacho kwa kupitia njia mbalimbali za kuwaendeleza (professional development). Viongozi hawa wanaongoza kwa mifano wakiwezesha vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake wa kuimarisha utawala wa kidemokrasia.

Kwa upande mwingine, watu katika taifa lolote wanaponyimwa haki na uhuru wao wa kupata habari husababisha kuenea kwa taarifa za upotoshaji, uvumi na dhana potovu.

Marekani ina fahari kubwa kushirikiana na vyombo vya habari vya Tanzania katika jitihada za kuwapatia Watanzania taarifa sahihi na zinazotolewa kwa wakati na kuhimiza na kuimarisha demokrasia.  

Vyombo vya habari vinashiriki kikamilifu na kuchangia katika kuweka kumbukumbu ya jitihada za kujenga demokrasia kwa kupitia chaguzi za kidemokrasia, mjadala wa katiba mpya na hata harakati za kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika kufanya maamuzi. Kuendelea kuimarika kwa uongozi na viwango vya utendaji katika vyombo vya habari kutawezesha kulinda mafanikio yaliyofikiwa na kupatikana kwa mafanikio zaidi katika nyanja hizi na nyinginezo.

Wakati siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikikaribia, Marekani inapenda kusisitizia dhamira yake ya dhati ya kuona kuwa waandishi huru wa habari wanafanya kazi yao bila hofu yoyote. 

Aidha, tunawakumbuka na kuwaenzi waandishi wa habari, waandishi katika mitandao (bloggers) na raia jasiri ambao wamejitolea maisha, afya na uhuru wao ili watu wengine waweze kufahamu ukweli. Hali kadhalika, tunathamini na kuenzi mchango wa vyombo huru vya habari katika kujenga demokrasia, uwazi na uthabiti wa jamii.

Tunatambua kuwa, kama wakala wa mabadiliko, viongozi wa vyombo vya habari wanachangia pia katika kuimarisha utawala bora na maendeleo ya kiuchumi kwa kujenga jukwaa litakalowawezesha wanajamii kutoa sauti yao na hivyo kuwezesha kujengwa na kukua kwa jamii iliyo wazi zaidi. 

Mjadala wa kitaifa nchini kote Tanzania utaimarishwa pale ambapo kila raia atasaidia kuiimarisha kada ya uandishi wa habari katika misingi ya maadili na uhuru na hivyo kuiwezesha kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa.

 Tunawapongeza waandishi wa habari wa Tanzania kwa kujitoa kwa dhati katika kuitumikia kada hii, ambayo ni mojawapo kati ya kada muhimu na zinazoheshimika duniani na tunaahidia kuendelea kuwapa ushirikiano wetu katika kufanikisha jitihada na maono yao.

Mwisho, kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi. Hillary Clinton, ni lazima tukumbuke kuwa katika maeneo mbalimbali duniani bado waandishi wa habari wanakabiliwa na vitendo vya unyanyasaji, ukatili na wakati  mwingine kuuawa. 

Leo hii tunakumbuka kuwa uandishi wa habari ni wito wa mashujaa wa kila siku. Ni lazima tuendelee kusimama kidete na kuwatetea wale wanaosimama na kupaza sauti zao katika mazingira hatari wanapotekeleza wajibu wao wa kutafuta, kurekodi na kufichua ukweli.
____________________________________________________________________
Dana L. Banks ni Afisa wa Masuala ya Umma wa Ubalozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

No comments: