Presidaa wa Ngwasuma, Nyosh akizungumza na wanahabari jijini Dar. |
BENDI ya muziki wa dansi ya Mashujaa Musica
'Wazee wa ibega' inatarajia kupamba uzinduzi wa albamu ya 'Chuki ya Nini'
ya bendi ya FM Academia utakaofanyika Desemba 21 mwaka huu jijini Dar es
Salaam.
Hayo yalisemwa jana Rais wa bendi hiyo, Nyoshi
El-Saadat alipokuwa akizungumza na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya
habari kuhusu maandalizi ya uzinduzi huo aliodai kuwa utakuwa wa kishindo.
"Hii ni albamu yetu ya kumi ambayo
imeandaliwa kwa ubora wa kimataifa na sasa iko tayari kuzinduliwa Desemba
21 tukisindikizwa na bendi ya Mashujaa Musica," alisema Nyoshi.
Nyoshi alitaja nyimbo za albamu hiyo kuwa ni
'Fataki', 'Otilia', 'Ndoa ya Kisasa', 'Neema', 'Dai Chako Ulaumiwe', 'Maisha',
'Madudu', 'Miraessa' na 'Intro' ambazo zote zimeshaingizwa kwenye video.
Aliongeza kusema kuwa katika uzinduzi huo
watawakumbuka pia kwakuwaombea watu wawili maarufu waliofariki dunia ambao ni
Rais wa zamani wa Afrika Kusini mzee Nelson Mandela na mwanamuziki mkongwe
wa Kongo, Tabu Ley.
Bendi ya FM Academia ilizindua albamu ya kwanza
ya 'Hadija' mwaka 1998 kisha ikafuatia ya pili iitwayo 'Atomic'
iliyozinduliwa mwaka 1999 na baadaye mwaka uliofuata wa 2000 bendi hiyo
ilizindua albamu ya tatu iliyopewa jina la 'Prison'.
'Wazee wa Ngwasuma' hawakuishia hapo, mwaka
2001 walizindua albamu ya nne iitwayo Freedom na kufuatiwa na ya tano ya
'Mpambe Nuksi' iliyozinduliwa mwaka 2001 na kisha ikafuata ya sita iitwayo
'Dotnata' mwaka 2003 kabla ya 'Dunia Kigeugeu' iliyozinduliwa mwaka 2006.
Baada ya hapo bendi hiyo ilikaa kidogo hadi
mwaka 2010 ilipozindua albamu mbili kwa mpigo ambazo ni 'Vuta Nikuvute' na
'Heshima kwa Wanawake' na sasa mwaka huu wa 2013 unaumalizia kwa
kuzindua albamu ya 'Chuki ya Nini'.
No comments:
Post a Comment