Na Jumbe Ismailly, Singida
MAHAKAMA ya Hakimu mkazi wilaya ya Singida imemuhukumu, Samweli Simon (22) mkazi wa Kijiji cha Ihanja, katika wilaya mpya ya Ikungi adhabu ya kutumia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukiri kosa la kumlawiti kijana wa kiume mwenye umri wa miaka tisa (jina tunalo).
Kijana huyo mdogo wa kiume aliyelawitiwa ni mkazi wa Kijiji cha Nkhoiree,tarafa ya Ihanja,katika wilaya hiyo mpya ya Ikungi.
Awali Mwendesha Mashitaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Bwana Shukurani Magafu alidai kwamba Juni12 mwaka huu katika muda ambao haujafahamika, mshitakiwa huyo alimlawiti mvulana huyo mwenye umri mdogo na hivyo kumsababishia maumivu makali kwenye sehemu yake ya kutolea haja kubwa.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Bi Terrysophia Tesha, Mwendesha mashtaka Bwana Magafu alidai kuwa siku ya tukio mshitakiwa alimlaghai kijana huyo na kisha kuingia naye ndani ya chumba chake cha kulala na baada ya kumvua kaptula,alimkaba kwa nguvu na kuanza kumwingilia kinyume na maumbile.
Alidai Mwendesha mashtaka huyo kwamba wakati mshitakiwa akiendelea na unyama wake ndipo kijana huyo alianza kupiga kelele ambazo zilichangia majirani na watu waliokuwa karibu na eneo la tukio kufika haraka kwa lengo la kujua kinachomsibu kijana huyo.
"Hata hivyo watu walipofika kwenye eneo la tukio walimkuta mshitakiwa bado akiendelea kuvaa suruali yake na ndipo walipomkamata na kumfunga kwa kamba ya katani inayotumika kufungia ng'ombe na kasha kumpeleka kituo kidogo cha polisi Ihanja",alifafanua Mwendesha mashitaka huyo.
Aidha mwendesha Mashtaka huyo alidai pia kuwa mshitakiwa alipofikishwa kituo cha polisi Ihanja bila kusumbua kwani alaiweka bayana unyama huo aliomtendea na kukiri kuwa ni kweli amemwingilia kimwili kijana huyo kinyume na maumbile.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo,Mwendesha mashtaka Bwana Magafu alidai kwamba pamoja na mshitakiwa huyo kutokuwa na rekodi yeyote ile ya makosa ya uhalifu lakini kitendo alichomfanyia mtoto huyo mdogo hakivumiliki mbele ya jamii.
"Mheshimiwa hakimu makosa ya aina hii yameendelea kushamiri katika Mkoa wetu,kwa hiyo naiomba Mahakama yako tukufu impe adhabu kali mshitakiwa ili iwe fundisho kwake na wakati huo huo iwaogofye watu wanaotarajia kufanya makosa ya aina hii",alisisitiza Mwendesha Mashtaka huyo.
Kwa upande wake mshitakiwa aliiomba mahakama hiyo imwonee huruma na kumwachia huru kwa kile alichodai kwamba amefanya kosa hilo kwa kusukumwa na pombe nyingi aliyokuwa amekunywa kwa siku hiyo.
Hata hivyo mshitakiwa huyo alisisitiza kwamba msamaha huo uzingatie kwamba yeye hakuisumbua Mahakama na pia hilo ni kosa lake la kwanza tangu alipozaliwa.
Akitoa hukumu hiyo,Hakimu wa Mahakama hiyo,Bi Tesha alisema sheria inamtaka kila mtu hapa duniani kumlinda mtoto ye yote dhidi ya madhara ya aina mbalimbali.
Alisema pia kuwa lakini mshitakiwa Samwel ameshindwa kumlinda mlalamikaji na badala yake ameamua kumfanyia unyama wa hali ya juu.
Kutokana na unyama huo aliomfanyia kijana huyo mwenye umri mdogo kwa hali hiyo Mahakama hiyo haina njia nyingine ye yoye ile ya kumuonea huruma,zaidi ya kumhukumu kwenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka 30 ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wanaotarajia kufanya kosa kama hilo.
No comments:
Post a Comment