Tangazo

June 19, 2012

Dewji kutumia zaidi ya Milioni 250/- kuboresha Mradi wa Kilimo Kwanza Singida

Mbunge wa jimbo la Singida mjini, Mh. Mohammed Gullam Dewji akihimiza kilimo cha Choroko, Dengu na Mbaazi kwa wakazi wa kitongoji cha Mtisi kata ya Mtamaa. Mbunge huyo ambaye alikuwa kwenye ziara ya kikazi jimboni kwake ambapo pamoja na mambo mengine, alisema mazao hayo yatawakomboa wapiga kura wake kiuchumi.(Picha na Nathaniel Limu).
**********************
Na Mwandishi wetu
Mbunge wa jimbo la Singida mjini (CCM) Mh. Mohamed Gullam Dewji anatarajia kutumia zaidi ya shilingi 250 milioni kugharamia mradi wa kilimo cha choroko, dengu na mbaazi katika msimu ujao wa ujao.

Mh. Dewji ambaye pia ni MNEC wa mkoa wa Singida, amesema hayo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kisima cha maji cha kitongoji cha Mtisi, kijiji cha Mtamaa.

Amesema fedha hizo zitatumika kununua tani 60 za mbegu hizo, kutoa mafunzo ya kilimo bora na ununuzi wa plau za kukokotwa na ng’ombe.

Amesema lengo la mradi huo  ni kuwajengea mazingira mazuri wakulima wa jimbo lake, kuboresha hali zao za kiuchumi.

“Mimi, madiwani pamoja na watendaji, tutawahamasisha wakulima kila kaya ilime ekari moja ya mazao hayo ya mbaazi, dengu na choroko.  Mazao hayo yana soko la uhakika na bei zake zipo juu zaidi ya zao la mahindi” amesema na kuongeza;

“Mimi binafsi nitanunua mazao hayo kwa bei ambayo itakuwa na faida kubwa kwa mkulima wa mazao hayo”.

Kuhusu plau, amesema majembe hayo ya kukokotwa na ng’ombe kila kikundi cha wakulima 25, watapatiwa plau moja bure.

Katika hatua nyingine, Mh. Dewji amesema mtaalam wa kilimo katika ofisi yake kwa ushirikiano na wataalam wa manispaa, watasimamia mradi huo kwa karibu, ili wakulima waweze kuzingatia ushauri wa kilimo bora.

“Lengo ni kwamba mavuno katika ekari hiyo moja ya aidha, dengu, choroko au mbaazi, yakidhi mahitaji ya kuweza kumkomboa mkulima kiuchumi”,amesema kwa kujiamni.

Wakati huo huo, mbunge huyo  alitumia nafasi hiyo kuwataka wakulima kubadilika na kuachana na kilimo cha mazoea na kuanza kulima kilimo kinachozingatia ushauri wa taalamu.

Aidha, amesema kutokana na misimu ya mvua za miaka hii kutokueleweka vizuri, njia pekee ya kunufaika na kilimo, ni mkulima kuwahi kuandaa mashamba na mbegu bora kabla msimu haujaanza.

No comments: