Tangazo

May 29, 2012

Mzee Iddi Simba Kortini kwa 'Ufisadi'

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), Iddi Simba (pichani) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kulitia hasara ya zaidi ya Shilingi Milioni 300 shirika hilo.

Simba alitinga Mahakamani hapo leo mwenyewe na tuhuma hizo zinamkabili yeye na wenzake wengine wawili wanaotuhumiwa pamoja.

Simba aliyewahi kuwa Waziri katika awamu ya pili na yatatu anakuwa niWaziri wa tatu mstaafu kufikishwa Mahakamani hapo kwa tuhuma za kuitia Hasara Serikali na Mashirika.

Sakata la Ufisadi UDA lilianza hivi

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilisema hivi karibuni kuwa, mkataba wa uuzwaji wa hisa za Serikali ndani ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ni batili na kwamba fedha zote zipo kwenye akaunti ya kada wa Chama Cha Mapinduzi na mwanasiasa wa siku nyingi Idi Simba, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo na kwa sasa bwana Simba ni mwenyekiti wa baraza la wazee wa mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza muda mfupi na waandishi wa habari  mjini Dodoma, baada ya kampuni iliyodai kununua shirika hilo kutoa taarifa kwa vyombo vya habari mjini hapa kuhusu ununuzi wa UDA, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, Kabwe Zitto alisema ununuzi huo ni batili.

“Niwape tu ufafanuzi wa jambo hili, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma ndiyo yenye jukumu la kusimamia sera ya ubinafsishaji, na kwa ufuatiliaji wetu, tumebaini kuna taratibu za kisheria zimekiukwa, na huyu mtu anayedai amenunua UDA, afahamu tu kwamba ametapeliwa, UDA bado ni shirika la umma”,alisema Zitto.

Aliongeza kuwa kammpuni ya Simon Group inayodai imenunua hisa asilimia 52 ya shirika hilo, imetapeliwa na kwamba fedha shilingi milioni 300 kati ya fedha shilingi milioni 760 wanazodai wamesha wekeza kwenye shirika hili, ziliwekwa kwenye akaunti ya mtu binafsi.

Alisema fedha hizo zimewekwa kwenye akaunti tofauti ya Idd Simba. Alizitaja akaunti hizo na tarehe ambazo fedha hizo ziliwekwa, ambapo katika benk M tawi la Sea View jijini Dar es Salaam, Septemba 2 mwaka 2009, fedha shilingi milioni 250 ziliwekwa kwenye akaunti binafsi ya Idd Simba .

Aidha, katika benki ya NMB tawi la Makambako, Novemba 26, mwaka 2009 fedha shilingi milioni 30 ziliwekwa kwenye akaunti binafsi ya Idd Simba, na Desemba 9,mwaka 2009 katika benki ya NMB tawi la Mlimani City shilingi milioni 20 ziliwekwa benki na kuingia kwenye akaunti ya Idd Simba tawi la Pride Songea Desemba 18, mwaka huo.

Zitto alisema kwa uchunguzi wa kamati hiyo kuhusu mwenendo mzima wa ubadhirifu wa shirika hilo, wamemwagiza CHC kufuatilia shirika la UDA na kuhakikisha hakuna mali yoyote ya shirika hilo itabadilishwa jina au kumilikiwa na mtu yoyote bila utaratibu wa sheria za ubinafshishaji.

No comments: