Tangazo

June 1, 2012

WALIOTAKA KUMWONDOA ASKOFU DK. MDEGELA WAKWAMA

Dk. Mdegela akitoa baraka zake. Kushoto ni Askofu Dk. Shayo.
PAMOJA na upepo wa amani ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa kuendelea kutokuwa shwari, Askofu Mkuu wake, Dk Owdenbug Mdegela amefanikiwa kuuzima moto uliomtaka aachie ngazi kutokana na tuhuma za kimaadili zinazomkabili.

Katika kikao cha Halmashauri ya Dayosisi hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Huruma Centre juzi mjini hapa Askofu Mdegela aliwaambia wajumbe wake kwamba atakabidhi madaraka yake kwa Askofu mpya wa dayosisi hiyo Oktoba 7, 2016.

Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho waliodai kuchukizwa na uamuzi wa Askofu huyo walisema watamuomba Mkuu wa Kanisa Askofu Alex Malasusa kuingilia kati suala hilo lililopata kujadiliwa katika kikao cha Baraza la Maaskofu wa Kanisa hilo.

Katika baraza hilo lililofanyika Machi 15, mwaka huu mkoani Morogoro chini ya Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Malasusa, baadhi ya tuhuma za kimaadili zinazodaiwa kumkabili Askofu Mdegella zilijadiliwa kwa kina na mapendekezo kutolewa.

Taarifa zilizothibitishwa na mmoja wa wajumbe wa baraza hilo (jina linahifadhiwa) zimedai kwamba Askofu Mdegella alipewa mwezi mmoja tangu tarehe ya baraza hilo (machi 15) awe ameitisha Halmashauri Kuu ya dayosisi yake na atumie busara kuachia ngazi.

Baadhi ya wachungaji walioshiriki kikao cha Halmashauri ya Dayosisi hiyo juzi, waliwaambia waandishi wa habari kwamba kwa kipindi kirefu kumekuwepo na tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwa askofu huyo, nyingi kati yake zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari mwaka jana.
Askofu Dk. Mdegela

Mmoja wa wachungaji hao aliyejitambulisha kwa jina la Kikoti alisema kama Askofu Mdegella angemuomba ampe ushauri, usingekuwa mwingine zaidi ya kumshauri ajiuzulu nafasi yake hiyo ili kulinda heshima yake ndani ya kanisa.

“Mvutano ni mkali sana, wengi wa wajumbe hawaungi mkono mapendekezo ya Baraza la Maaskofu yanayotaka ajiuzulu kwasababu ya tuhuma mbalimbali zinazomkabli,” alisema.

Alisema mgawanyiko huo unampa fursa Askofu Mdegela wa kuendelea na wadhifa wake kwa kuwa wenye maamuzi ya mwisho dhidi ya Askofu wao ni wajumbe wa vikao halali vya dayosisi hiyo.

Kwa upande wake Muinjilisti Hopeman Kihonza alisema aliachishwa masomo ya uchungaji baada ya kutoa ushirikiano kwa kamati ya maaskofu watatu waliokuwa wakichunguza tuhuma zinazomuhusu askofu huyo.

Akiwa mmoja kati ya waumini tisa waliohojiwa na maaskofu hao watatu Dk Martin Shao, Dk Hans Mwakabana na Elisha Buberwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili Askofu Mdegela, Muinjilisti Kihonza alisema aliamriwa aondoke kwenye kituo cha mazoezi Usharika wa Nyanzwa, wilayani Kilolo kabla ya Februari 28, mwaka huu.

Katika barua ya kuachishwa masomo ya uchungaji iliyosainiwa na Askofu Msaidizi Blaston Gavile kwa niaba ya Askofu Mdegela (nakala tunayo), Kihonza alisema alifutiwa dhamana na ufadhili wa masomo ya uchungaji katika Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa baada ya kutoa ushahidi wake kwa maaskofu hao watatu Januari 10, mwaka huu.

Hata hivyo mara kadhaa Askofu huyo amenukuliwa akikanusha tuhuma zote zinazoelekezwa dhidi yake.

Wakijadili ajenda ya nne katika kikao cha halmashauri ya dayosisi hiyo juzi, Askofu Mdegella anadaiwa kuwataja waumini sita wa kanisa hilo akiwemo Hopeman Kihonza na Obeid Mtatifiko wanadaiwa kuwa vinara wa mtandao wa kumkashifu.

Katika kikao hicho Askofu Isaya Mengele wa Dayosisi ya Kusini na Askofu Jacob Mbwilo wa Dayosisi ya Matamba walihudhuria kama wawakilishi wa Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Malasusa.

Ajenda zilizojadiliwa (nakala tunayo) ni pamoja Kufungua Mkutano, Kuangalia Mahudhurio, Ajenda Maalumu inayomuhusu Askofu wa Dayosisi wa Iringa, Vinara wa Mtandao wa kumchafua askofu huyo, Udhibiti na Mustakabali wa kidayosisi na Kufunga mkutano.
 Habari na picha kwa hisani ya Francis Godwin Blog

No comments: