Tangazo

July 24, 2012

ATAKA WAZIRI WA ZAMANI WA MIPANGO WA RWANDA AFUNGWE MAISHA

Na Hirondelle, Arusha

Arusha, Julai  24, 2012 (FH) – Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumatatu ameiomba mahakama hiyo kumpatia adhabu ya kifungo cha maisha jela Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda, Augustin Ngirabatware iwapo atatiwa hatiani kwa kuhusika na mauaji hayo mwaka 1994.

Akitoa sababu kwa nini Waziri huyo apewe adhabu kali kiasi hicho, Mwendesha Mashitaka, Rashid Rashid alisema ‘’kutokana na ushahidi ulitolewa mahakamani, nia ya Ngirabatware ya kutekeleza mauaji ya kimbari imethibitishwa pasipo mashaka.’’

Mwendesha Mashitaka alikuwa anatoa hoja za mwisho katika kesi hiyo, mbele ya mahakama iliyokuwa inaongozwa na Jaji William Sekule. Alifafanua kwamba Ngirabatware alitenda uhalifu wa kutisha na kushiriki katika njama za uhalifu huo kwa kushirikiana na watu wengine.

‘’Alitekeleza, kuandaa,kuchochea, kuhimiza, kusaidia na kupiitisha adhma ya mauaji dhidi ya raia wa Watutsi.Ametekeleza uhalifu huo katika wilaya alikozaliwa ya Nyamyumba, mkoa wa Gisenyi, Kaskazini mwa Rwanda,’’ mwendesha mashitaka alisema.

Rashid alilikumbusha jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo kuwa walisikiliza ushahidi wa siku moja baada ya kutunguliwa kwa ndege ya Rais Junvenal Habyarimana Aprili 6, 1994 na kusababisha kifo chake kwamba mshitakiwa alikwenda wilayani kwake ambako alidaiwa kupeleka silaha.

Mwendesha mashitaka iliendeela kufafanua kwamba, Ngirabatware kama Waziri katika seriklai ya mpito, mjumbe wa chama tawala cha MRND katika ngazi ya mkoa na mkwe wa mfanyabiashara maarufu, Felicien Kabuga, ambaye ndiye anayesadikiwa kufadhili mauaji ya kimbari, alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa katika wilaya na mkoa wake.

‘’Alihakikisha kwamba Faustine Bagango, anachaguliwa kuwa meya wa wilaya yake na kuwa kitivo cha utekelezaji wa mauaji dhidi ya Watutsi. Walikuwa na malengo sawa. Alimtumia kusambaza silaha pamoja na kupanga na kuwaongoza wanamgambo wa Interahamwe kuua Watutsi,’’ alieleza.

Rashid aliongeza, ‘’Ngirabatware hakutaka tena kuona Mtutsi yoyote katika wilaya ya Nyamyumba,’’

Waziri huyo wa zamani anashitakiwa kwa kula njama za kufanya mauaji ya kimbari, mauaji ya kimbari au kushiriki mauaji hayo, uchochezi, kuteketeza kizazi na ubakaji kama uhalifu dhidi ya binadamu.

Uwasilishaji wa hoja za mwisho unaendelea Jumanne.

No comments: