Tangazo

September 20, 2012

AIRTEL Tanzania yaipiga Jeki Rock City Marathon 2012

Afisa Uhusiano wa kampuni ya Airtel Tanzania, Bi. Jane Matinde (kulia) akimkabidhi mfano wa hundi ya Milioni 5/- Meneja Matukio wa kampuni ya Capital Plus International, ambaye pia ni Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon 2012, Bi. Grace Sanga jijini Dar es Salaam jana kama sehemu udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza tarehe 28 Oktoba. Airtel pia walikabidhi T-sheti 400 ili kusaidia mbio hizo.
********
KAMPUNI ya mawasiliano nchini ya Airtel imeahidi kuendelea kusaidia michezo mbalimbali nchini ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya vijana.

 Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya kukabidhi shilingi milioni tano pamoja na fulana mia moja kama udhamini wa mbio za Rock City Marathon za mwaka huu zenge kauli mbiu ‘tukuze utalii wa ndani kupitia michezo’, Afisa Uhusiano wa Airtel, Bi Jane Matinde alisema kuwa kampuni yake itaendelea kusaidia michezo mbalimbali nchini ikiwemo riadha ili kukuza maendeleo ya vijana.

 “Udhamini wetu wa shilingi milioni tano pamoja fulana mia moja katika mbio za Rock City mwaka huu unalenga katika kusukuma maendeleo ya vijana kupitia michezo kwa tunaamini kuwa michezo imekuwa ni chanzo kikubwa cha ajira duniani.

 “Tunaahidi kuendelea kusaidia michezo mingine kwa kuwa pia tunaamini kupitia michezo mbalimbali tunaweza kutangaza vivutio vyetu vya utalii duniani. Mfano nzuri ni mbio za mwaka huu za Rock City Marathon zitakazowakutanisha wanariadha mbalimbali kutoka nchi jirani,” aliongeza Bi. Matinde.

 Akipokea hundi na fulana hizo, Mratibu wa mbio hizo kutoka katika kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bi. Grace Sanga aliishukuru kampuni ya Airtel kwa kuendelea kusaidia mbio za Rock City na kuyahasa mashirikia na makampuni mengine kuiga mfano wa kampuni hiyo.

 “Tunaishukuru Airtel kwa msaada wao kwa kuwa msaada huu utatusaidia tujiandae vizuri na Rock City Marathon ya mwaka huu itakayofanyika Oktoba tarehe 28 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza,” alisema Grace.

 Grace alisema kuwa mbali na Airtel wadhamini wengine ni pamoja na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Parastal Pension Fund (PPF), Geita Gold Mine, African Barrick Gold, Air Tanzania Company Ltd (ATCL), Mamlaka ya Taifa ya Mbuga za Wanyama nchini (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nyanza Bottles, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.

 Aidha, Bi Sanga aliwaasa wanariadha kujitokeza na kuanza kujisajili ili kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa fomu za usajili zinapatikana katika ofisi za uwanja wa CCM Kirumba, ofisi za kampuni ya Capital Plus International zilizopo katika jengo la ATCL ghorofa ya tatu, ofisi za Bodi ya Utalii jengo la IPS ghorofa ya tatu, Dar es Salaam, na zinapatikana katika tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot.com.

 CPI ilitangaza kuwa atakaeibuka kinara katika mbio za kilometa 21 mwaka huu kwa wanaume na wanawake atazawadiwa shilingi milioni moja na laki mbili wakati mshindi wa pili ataweka mfuko shilingi laki tisa na mshindi wa tatu ataondoka na shilingi laki saba.


No comments: