Tangazo

September 3, 2012

MAMIA WAMZIKA KATIBU WA CCM MOROGORO

Vijana wa CCM wakibeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, Asha Kipangula, wakati wa mazishi yaliyofanyika leo nyumbani kwa marehemu, Iringa. Marehemu Kipaungula alifariki dunia juzi mjini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU, IRINGA

MAMIA ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi kwa jumla wamejitokeza kumzika kwa heshima zote aliyekuwa Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, marehemu Asha Kipangula.

Asha Kipangula (48) aliyefaliki juzi mjini Dar es Salaam, amezikwa leo katika makaburi ya Mlolo mjini Iringa katika maziko yaliyoongozwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye.

Pamoja na Nape pia wamehudhuria viongozi mbalimbali wa Chama na serikali, wakiwemo Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba, wakuu wa mikoa Joel Bendera (Morogoro), Dk. Christina Ishengoma (Iringa), Saidi Mwambungu (Ruvuma), Kandoro na wa CCM na wabunge kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Morogorona Iringa.
 
Akizungumza kwenye Msiba huo, Nape alisema, Chama Cha Mapinduzi kimepoteza kiongozi mchapakazi ambaye wakati wote alikuwa mstari wa mbele kutekeleza majuku yake ya kujenga na kuimarisha uhai wa Chama katika ngazi na maeneo yote aloyowahi kukitumikia Chama.

Katika uhai wake, Asha amewahi kuwa Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)  mkoa wa Iringa,  Katibu wa CCM wilaya ya Makete mkoani humo na Katibu wa CCM mkoa wa Ruvuma, Tabora na Morogoro ambako mauti yamemkuta akiwa mkoa huo.

Nape alisema, kufuatia msiba huo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Rais jakaya Kikwete ameipa pole familia ndugu na jamaa wa marehemu Asha na viongozi na wanachama wa CCM kwa jumla.

Amesema kutokana na kuguswa na msiba huo, Chama makao makuu kimetoa ubani ambao itapewa familia ya marehemu. CCM ngazi za mikoa na wilaya katika maeneo mbalimbali pia wametoa ubani.

Kwa upande wake, Makamba alisema, japokuwa kumlilia marehemu ni jambo la kawaida kwa binadamu kwa kuwa hata baadhi ya manabii wa Mungu walifanya hivyo, lakini kubwa zaidi ni kufuata nyayo za utendaji uliotukuka aliokuwa nao marehemu.

Amina ambaye amefariki Septemba 1, 2012 mjini Dar es Salaam, ameacha mtoto mmoja wa kiume na watoto watano wajane aliokuwa akiwalea.

No comments: