Tangazo

September 3, 2012

TAMKO LA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF), KUHUSU KUUAWA KWA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI

Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena
UTANGULIZI:

1. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.

2.Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa akiwa kazini jana, Septemba 2, 2012, wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

3.Tukio hili linaiingiza Tanzania katika historia mbaya ya ukiukwaji na ukandamizwaji wa uhuru wa habari, kwani ni kwa mara ya kwanza tunashuhudia mwandishi wa habari AKIUAWA WAKATI AKITEKELEZA MAJUKUMU YAKE YA KIHABARI.

4. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Mwangosi kabla ya kufikwa na mauti saa 9.30 alasiri katika kijiji cha Nyololo, Mufindi, alizingirwa na kushambuliwa na polisi waliokuwa katika eneo la tukio. Na hata alipopiga kelele za kuomba msaada, hakusikilizwa na matokeo yake aliuawa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.

5.Kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, TEF tumechukua hatua za haraka za kuunda timu ya uchunguzi wa suala hilo, ambayo itakwenda mkoani Iringa mapema kadri itakavyowezekana, ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi (documentation) ya tukio hilo la aina yake katika historia ya nchi yetu.

6. Matokeo ya uchunguzi huo pamoja na mwingine unaofanywa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ndiyo yatakayotoa mwelekeo wa hatua ambazo TEF inachukua dhidi ya Jeshi la Polisi katika siku chache zijazo.

MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF

Kwa kuzingatia taarifa kutoka Iringa na zile za vyombo vya habari vya jana (Jumapili, Septemba 02, 2012) na leo (Jumatatu, Septemba 03, 2012), TEF ina mtizamo na msimamo kama ifuatavyo:

1. Kwanza tunalaani vikali tukio la kupigwa, kisha kuuwawa kwa mwandishi Daudi Mwangosi ambalo limeigusa tasnia ya habari kwamba sasa pengine waandishi wa habari ni malengo “target ya polisi” wanapokuwa kwenye kazi zao.

2. Ieleweke wazi kwamba matukio haya siyo yanaondoa imani ya waandishi wa habari kwa jeshi la polisi tu, bali yanaweza kuwa chanzo cha uhasama na ufa mkubwa ambao utawanyima wananchi nafasi ya kutumikiwa na pande mbili ambazo zinategemeana.

3. Kwa matukio ya aina hii, tunadhani wakati mwafaka kwa uongozi wa Jeshi la Polisi nchini kuwajibika, kuazia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa na uongozi wa Makao Mkuu, akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema.

4.Tunasema hivi kwani kuna kila dalili kwamba polisi wanahusika kwa namna moja au nyingine na tukio au/na matukio yaliyosababisha kifo cha Mwangosi, kwani kitendo cha kumzingira tu na kumshambulia kinathibitisha kwamba hawakuwa na nia njema hata kidogo dhidi ya mwandishi huyu.

5.Taarifa ambazo TEF tunazo, pia  zinadai kwamba kulikuwa na mpango wa polisi wa “kuwashughulikia waandishi wa habari watatu” (Mwangosi) akiwa mmojawapo na hilo lilionekana likitekelezwa kwa polisi kumshambulia mwandishi huyo, baadaye alipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

6. Hili linatiliwa nguvu na tukio jingine la polisi kumpiga na kumjeruhi  mwandishi mwingine, Godfrey Mushi ambaye ni mwakilishi wa gazeti la Nipashe mkoani Iringa. Mwandishi wa tatu ambaye hadi tunapoandika taarifa hiyo yumo katika mpango wa ‘kushughulikiwa na polisi’ ni Francis Godwin ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea.

7. Vitendo vya aina hii havivumiliki na havipaswi kuachwa kuendelea kwani ni hatari kwa ustawi wa demokrasia na uhuru wa habari nchini. Hatuwezi kuendelea katika mazingira ambayo polisi wanageuka kuwa chombo cha mauaji ya raia badala ya kuwa walinzi wa raia.

8. Kwa maana hiyo, mbali na uchunguzi ambao utafanywa na polisi, tunatoa wito kwa Serikali kuunda chombo huru, ambacho kitabaini ukweli, na matokeo yake yatangazwe kwa umma, huku wahusika wa aibu hiyo wakichukuliwa hatua za kisheria. Tunasema hivyo, tukifahamu kwamba tayari kuna jitihada za kuficha ukweli na kueneza propaganda za uongo kuhusu tukio zima.

9. Mwenendo wa aina hii wa chombo cha dola kuamua kutumia silaha kuua na baadaye kupanga mbinu chafu za kuficha ukweli ni hatari kwa Taifa, na unaiweka demokraisia ya nchi yetu njia panda, huku tukielekea katika hatari ya Taifa kutumbukia katika uovu.

IMETOLEWA NA:

NEVILLE MEENA,
KATIBU MKUU – JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF)
SEPTEMBA 3, 2012

 

No comments: