Tangazo

September 3, 2012

Picha za Matukio mbalimbali yaliyopelekea Kifo cha Mwanahabari Daud Mwangosi



Askari (kushoto), anaonekana kumwelekezea mtutu tumboni.



Mabaki ya mwili wa Mwangosi.

Marehemu Daud Mwangosi enzi za Uhai wake.
***************************
VURUGU kubwa zimezuka katika eneo la Nyororo wilayani Mufindi kati ya polisi na wafuasi wa Chadema, baada ya askari hao kusambaratisha mkutano wa chama hicho na kusababisha kifo cha mwandishi wa habari na watu kadhaa kujeruhiwa.

Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi anadaiwa kuuawa kwa bomu lililorushwa na polisi katika vurugu hizo.

Awali, inadaiwa kuwa mwandishi huyo alishambuliwa kwa marungu na Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kabla ya bomu hilo kumjeruhi vibaya tumboni na kusababisha kifo chake.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio, alisema wakati mwandishi huyo akishambuliwa na polisi, mmoja wa askari wa jeshi hilo aliwazuia wenzake kuendelea kumpiga akiwaeleza kuwa anamfahamu kuwa ni mwandishi wa habari, huku akimkumbatia.

Shuhuda huyo alidai kwamba jitihada za askari huyo hazikusaidia, kwani baada ya kutupwa kwa bomu hilo lililosababisha utumbo wa mwandishi huyo kutoka nje, polisi huyo naye alijeruhiwa mguu.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alikana polisi kumuua mwandishi huyo akidai kwamba kilichosababisha kifo chake ni kitu kilichorushwa na wananchi ambapo alisema polisi inakichunguza.

“Mwandishi alikuwa akikimbia kutoka upande wa wananchi kuelekea walipokuwa polisi. Kuna kitu kilirushwa kikitokea upande wa wananchi na kumfikia ambacho kilimjeruhi pia askari akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS).” Hata hivyo, hakumtaja OCS huyo. 

Vurugu hizo ziliibuka baada ya polisi kufika Nyororo na kuwataka viongozi wa Chadema pamoja na wafuasi wao kutawanyika kwa kuwa walikuwa hawaruhusiwi kufanya mkusanyiko wowote kutokana na amri iliyotolewa na jeshi hilo awali.

Polisi mkoani Iringa jana asubuhi walilipiga marufuku kufanyika kwa maandamano na mikutano yote ya halaiki ya kisiasa mpaka hapo Sensa ya Watu na Makazi itakapokamilika baada ya kuongezwa wiki zaidi.
Hata hivyo, pamoja na amri hiyo Chadema kilifanya mkutano wilayani Mufindi kitendo ambacho polisi walisema ni kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alisema ambaye alikuwa akiongoza askari wake kuwatawanya wafuasi wa Chadema katika eneo hilo, alisema kazi yao ilikuwa ni kutekeleza amri akisema wao si wanasiasa. “Nataka watu wote mtawanyike,” alisema Kamanda Kamuhanda.

Hata hivyo, viongozi wa Chadema walikaidi amri hiyo wakisema kuwa walikuwa wanaendelea na mikutano yao ya ndani siyo ya hadhara, kauli ambayo polisi walikataa.

Kabla ya polisi kutaka kuwakamata viongozi hao, wananchi waliwazuia kufanya hivyo na hapo ndipo vurugu zilipoanza na mabomu ya machozi kupigwa kitu na kila mtu kutawanyika.

Katika vurugu hizo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Hamad Yusuf alikamatwa na mtu mwingine ambaye jina lake bado halijafahamika.

Jukwaa la Wahariri latoa tamko
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Nevile Meena amesema jukwaa linalaani kitendo cha polisi kuua mwandishi kwa sababu za kisiasa.

“Tunalaani sana kitendo kilichofanywa na polisi kuua mwanahabari kwa sababu za kisiasa.”

Awali
Jana asubuhi, Chadema kilikuwa ifanye maandamano na mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Mwembetogwa, Iringa ikiwa ni sehemu ya kampeni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko(M4C).

Hata hivyo, muda mfupi kabla ya kuanza maandamano hayo, Kamanda Kamuhanda aliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na kuongezwa kwa siku za Sensa ya Watu na Makazi, jeshi hilo limepiga marufuku kufanyika maandamano na mikutano yote ya kisiasa kwa vyama vyote nchini, ili kuepusha mwingiliano.

 “Polisi inasimamisha shughuli zote za maandamano na mikutano ya halaiki ya kisiasa nchini, hivyo hakuna mkutano wala maandamano yoyote yanayotakiwa kuwapo wakati wa zoezi hili na ndiyo maana nimewaita niweze kutoa taarifa ya kusitishwa kwa mikutano yote,” alisema Kamuhanda na kuongeza:

“Kwa msingi huo sasa lazima niseme kuwa Polisi katika hili haihitaji mjadala wowote ule, inahitaji wahusika watii agizo hili bila shuruti ili kuepusha msuguano usiokuwa wa lazima ambao utasababisha matumizi ya nguvu kutumika.”

“Endapo Chadema watakaidi agizo hili, Polisi italazimika kutumia uwezo wake kuhakikisha ya kuwa amri hii inafuatwa tena bila shuruti. Tupo tayari na tumejiandaa kikamilifu kuhakikisha amri hii inatimizwa kwa namna yoyote ile kwa hiyo ni vyema Chadema wakaliona hili.”

Baada ya kauli hiyo ya Polisi, Kamanda wa Operesheni Sangara inayoendesha M4C, Benson Kigaila alieleza kushangazwa kwake na jinsi Polisi kuingilia kati shughuli zao za kisiasa.

“Morogoro, Polisi walituzuia mikutano yetu kwa madai ya Sensa na baadaye wakasema maandamano na mikutano yetu mkoani humo yasifanyike kwa kisingizio kwamba barabara ni finyu.”

“Tulipofika Iringa tulipaswa kufanya mikutano yetu tarehe 28, lakini IGP alitupigia simu kutuomba kutofanya mikutano yetu na kimsingi tulikubana naye kuonyesha uzalendo kusitisha mikutano yetu mpaka Sensa itakapokamilika, lakini sasa baada ya hapo tena leo wametuzuia kuendelea na shughuli zetu.”

No comments: