Tangazo

October 22, 2012

TV ZENYE MIGONGO NA MATUMBO MAKUBWA PIA ZITAPOKEA MATANGAZO YA DIGITALI

Na Mohammed Mhina, Zanzibar

Imeelezwa kuwa TV zote zikiwemo zile zenye migongo, matumbo na viuno virefu zote zina uwezo sawa wa kupokea matangano ya digitali na Watanzania waepuke uvumi wa watu wachache wanaodai kuwa TV  za zamani hazitapokea zitafutwa mara Tanzania itakapoingia kwenye mfumo wa Digitali.

Wito huo umetolewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano hapa nchini TCRA ambaye pia na Mratibu wa Ofisi za Kanda Bw. Victor Nkya, wakati wa mkutano wa Wataalamu wa Mawasiliano ya Habadi kwa njia ya digitali kutoka nchi za SADC unaojadili umuhimu wa mfumo wa Digitali.

Bw. Nkya amesema kuwa wananchi hawana haja ya kuwa na hofu juu ya TV walizonazo zikiwemo zenye matumdo na migongo mikubwa kuwa hazitaweza kupokea matangazo ya televishen katika mfumo mpya wa digitali.

Amesema kutokana na watu wengi kutumia televishen za Analojia, ni lazima kila mmoja wetu awe na kingamuzi na kazi ya Mamlaka ya mawasiliano ni kuwajengea wananchi matumaini na kuepuka kudanganywa.

Kwa siku za hivi karibuni baada ya Tanzania kuridhia mabadiliko ya mfumo wa Digitali, wananchi wamekubwa na wasiwasi wakidhani kuwa huo ndio mwisho wa tv za zamani.

Awali akifungua Mkutano huo wa siku tatu hapa mjini Zanzibar, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Rashid Suleiman, amewataka wananchi kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa mabadiliko ya kutoka katika mfumo wa analojia na kuingia katika digitali.

Amesema ni vema wananchi wakahama mapema kutoka katika mfumo huo wa zamani ili kuepuka usumbufu wakati yatakapotokea mabadiliko hayo kwani hakutakuwa na muda wa nyongeza kama Watanzania walivyozoea.

Na kuna umuhimu wa wananchi pia kusikiliza maelekezo ya wataalamu badala ya kusikiliza propaganda za watu wasio na ujuzi juu ya teknolojia hiyo.

"Watanzania hawana haja ya kuogopa na badala yake wajiandae kujipatia vingamuzi na kinyume cha hivyo watashindwa kupata matangazo ya televishen kama wanavyotarajia." Alisema Waziri.

Amesema kila mabadiliko yana hasara na faida zake, lakini kwa mabadiliko ya kutoka katika mfumo wa analojia kwenda digitali, kuna faida kubwa na moja ya faida hizo ni kuwawezesha watu wote kupokea matangaza sawa na yenye ubora unaofanana na kwa wakati muafaka.

Mkutano huo wa siku tatu unazishirikisha nchi zote za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC ikiwemo  Angola, Afrika ya Kusini, Malawi, Namibia, Botswana, Swazlland, Lesotho, Msumbiji na wenyeji Tanzania.

No comments: