Tangazo

February 19, 2013

Vijana watakiwa kufanya kazi na kuijunga na vikundi vya Maendeleo

Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi

 Vijana wametakiwa kutumia muda wao kufanya kazi kwa kujituma na kujiunga na vikundi vya maendeleo  ili waweze kufikika kirahisi zaidi na kuwezeshwa kuichumi kuliko kutumia  muda huo  kwa kujihusisha na mambo yasiyoleta maendeleo.

Wito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa (NEC) ambaye pia ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipokuwa  akiongea na wanakijiji cha Kikwetu kilichopo kata ya Mbanja wilaya ya Lindi mjini wakati wa ziara yake ya kichama ya siku saba wilayani humo.

Mama Kikwete alisema kuwa  hivi sasa vijana wengi wamekuwa wakilaumu kuwa hakuna ajira jambo  ambalo ni kweli vijana wengi lakini ukiangalia kwa undani utaona kuwa hawafanyi kazi na kutumia  muda mwingi kucheza mchezo wa pool hasa nyakati za asubuhi.  Nawaomba  viongozi wa Serikali pangeni  utaratibu ili mchezo huo uchezwe nyakati za jioni.

“Licha ya kutokupenda kufanya kazi, baadhi ya vijana  wa kiume wanapenda kuwa na mahusiano ya kimapenzi na watoto wa shule yanayopelekea kupata ujauzito na kukatisha masomo yao, nawasihi muwaache mabinti hawa wasome kama kweli mnawapenda muwasubiri wanalize shule na kufuata taratibu ili muweze kufunga ndoa na siyo kuwachezea”, alisema Mama Kikwete.

Akiwa katika kata ya Rasbura aliwataka wakazi  wa kata hiyo  ambayo iko kandokando ya Bahari ya Hindi kujenga vyoo na kuvitumia kwani baadhi ya wananchi wanaoishi kandokando ya fukwe  hawapendi kutumia vyoo na kwenda kujisaidia fukweni na  kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.

Alisema, “Muwe na tabia ya kujenga vyoo na kuvitumia kwani ukienda kujisaidia baharini ni hatari kwa kuwa bahari haina tabia ya kutunza uchafu hivyo basi baada ya muda itautema uchafu wote nje katika fukwe na kusababisha magonjwa na uharibifu wa mazingira.

Akisoma taarifa ya kata ya Mbanja  diwani Hamidi Juma alisema kuwa idadi ya wananchi wanaofuga ng’ombe imeongezeka kutoka kaya 10 hadi 23 ambazo zinafuga ng’ombe 63 na kujiongezea kipato cha familia na hivyo kuwa na uhakika wa kujitapia chakula.

Kwa upande wa afya alisema kuwa licha ya kuwa na upungufu wa wahudumu wa afya katika kituo cha afya  bado watumishi waliopo  wanajitahidi kutoa  huduma nzuri kwa wananchi na katika siku za hivi karibuni hakuna vifo vya kina mama wajawazito na watoto vilivyotokea pia hakuna magonjwa ya milipuko yaliyowakumba wananchi.

Taarifa ya Kata ya Rasbura ilionyesha kuwa Serikali ilifanya zoezi la kukagua  nyumba 864 ili kuona kama zina vyoo na  kugundua kuwa nyumba  675 zina vyoo vinavyokubalika , vyoo vibovu 141 na nyumba ambazo hazina vyoo ni 68. Kati ya hivi vyoo vya kawaida ni 487, vya kumwagia maji ni 17 na vyoo vya shimo vyenye karo na bomba wima 360.

Serikali ya kata hiyo pia ilitoa elimu ya ufugaji wa kisasa kwa kumtembelea mfugaji mmoja mmoja nyumbani kwake na kufanikiwa kuwafikia wafugaji 23 wa ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda, nguruwe na kuku kwani kama mwananchi atafuga kitaalamu atajipatia pato la kutosha na hivyo kujikwamua kiuchumi.

Katika mkutano wa kijiji cha Kikwetu  Mjumbe huyo wa NEC aliwapokea vijana 25 na mzee mmoja waliokuwa wanachama wa CUF na kujiunga  na CCM. Akiwa katika kata za Mbanja, Rasbura na Mwenge alikabidhi  kadi  kwa wanachama  wapya wa CCM  31, Umoja wa vijana 101, Umoja wa Wanawake  75 na Jumuia ya Wazazi  22.

No comments: