Tangazo

April 2, 2013

DC ashauri 'Niache Nisome' iwe taasisi kuwalinda wasichana kielimu

Na Thehabari.com, Handeni

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu ameshauri kampeni aliyoianzisha wilayani humo yenye kauli ya 'Niache Nisome' kupambana na mimba kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa elimu, iwe taasisi na kufanya shughuli zake nchi zima.

Rweyemamu aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi juu ya hali ilivyo kwa sasa ya matukio ya mimba kwa wanafunzi na kukatishwa masomo, vitendo ambavyo alivikuta vikishamiri eneo hilo hasa mwanzoni mwa mwaka jana kabla ya uteuzi wa nafasi hiyo.

Akizungumzia kampeni ya 'Niache Nisome' aliyoianzisha muda mfupi baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuiongoza wilaya hiyo, alisema kampeni yake imekuwa na mafanikio kwani licha ya matukio ya mimba kupungua wananchi wameipokea vizuri kampeni hiyo.

Alisema wananchi hasa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiripoti matukio ya mimba na kutoa ushirikiano pale inapoitajika ili wavunjaji sheria kwa wanafunzi waweze kuadhibiwa kitendo ambacho hapo awali kilikuwa kigumu, na hata wengine kushirikia mikakati ya kuwaachisha masomo wanafunzi.

"Nina furahi kuwa muitikio wa kampeni ya 'Niache Nisome' katika maeneo mengi ya wilaya yangu imepokelewa vizuri, wananchi wanaanza kutambua umuhimu wa elimu na wanatoa ushirikiano kwa wale wachache wanaokwenda kinyume kwa kuwakatisha masomo wanafunzi hasa wa kike...jamii ya hapa wengi wao mwanzoni ilikuwa ni kitu cha kawaida mwanafunzi kulala nje pasipo idhini ya wazazi wake," alisema Rweyemamu akizungumza.

Akizungumzia utekelezaji wa kampeni hiyo Mkuu wa wilaya alisema licha ya kamatakamata iliyokuwa ikifanyika kwa wazazi, wanafunzi na watu waliyokuwa wakisababisha mimba kwa wanafunzi viongozi na watendaji anuai wa halmashauri hiyo walizunguka maeneo mengi na kutoa elimu juu ya umuhimu wa elimu kwa jamii zima.

"Tulikamatana sana mwaka jana kuanzia mwezi wa nane na kwa muda mfupi tulikuwa tuna watuhumiwa 80 wakiwemo wazazi, watu waliokuwa wakidaiwa kusababisha mimba kwa wanafunzi pamoja na wanafunzi wenyewe...mimi mwenyewe nilitembelea baadhi ya shule nikitoa elimu lakini baadaye walielewa licha ya uwepo wa changamoto kadhaa," alisema kiongozi huyo wa Wilaya ya Handeni.

Aidha akifafanua zaidi alisema ipo haja ya kampeni hiyo kugeuzwa taasisi na kuanza kufanya shughuli zake nchi nzima ili kampeni kama hiyo iweze kuyanufaisha maeneo mengi ambayo yamekuwa na mwamko duni wa elimu kwa jamii. Aliongeza kuwa faida ya kampeni hiyo haipiganii elimu kwa mtoto wa kike pekee kwani inagusa maeneo mengine pia kama miundombinu ya shule, vitendea kazi na vifaa vingine muhimu kwa shule kiujumla.

Hata hivyo kiongozi huyo alisema licha ya kuanza kufanikiwa katika kampeni hiyo bado suala la ufauli katika shule za sekondari hasa kidato cha nne ni tatizo kutokana na ilivyokuwa hapo awali. Alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana (2012) yalikuwa mabaya sana kwani Wilaya nzima ya handeni haikuwa na daraja la kwanza.

"changamoto iliyobaki sasa ni ufaulu...matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka jana wilaya nzima ilikuwa na ziro 246, hatukuwa na daraja la kwanza kabisa huku tukipata wanafunzi 2 tu walio na daraja la pili," alisema Rweyemamu.

Mwezi Machi mwaka jana Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kilifanya utafiti wa kihabari Wilayani Handeni kuangalia matukio ya mimba kwa wanafunzi na kubaini uwepo wa kesi nyingi za wanafunzi kutiwa mimba na kukatishwa masomo.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA

No comments: