Tangazo

July 24, 2013

Mama Kikwete awataka viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kuhubiri amani

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoa nasaha zake baada kuwafuturisha viongozi wa serikali, madhehebu ya dini wa wilaya ya Mkuranga na wananchi wa kijiji cha Hoyoyo kilichoko karibu na Mkuranga katika Mkoa wa Pwani tarehe 23.7.2013. PICHA/JOHN LUKUWI

Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,WAMA, Mama Salma Kikwete akifanya mazungumzo na Mama Cherrie Blair, Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza walipokutana kwenye ofisi za WAMA tarehe 23.7.2013. Mama Blair yupo nchini akifuatana na mumewe Tonny Blair katika ziara ya kikazi.

Sehemu ya waalikwa katika futari hiyo.
Na Anna Nkinda  - Maelezo

Viongozi wa dini  nchini wametakiwa kuhubiri amani katika majukwaa yao  ili jamii ielewe umuhimu wa kuwepo kwa amani na kuendelea kuishi kwa   upendo na ushirikiano.

 Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwafuturisha wanakijiji cha Hoyoyo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Mama Kikwete alisema kuwa viongozi wa dini wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa waumini wao wanaelewa umuhimu wa amani katika nchi kwa kujenga mshikamano kama waasisi wa Tanzania walivyouanzisha .

“Katika shughuli yetu hii tumekusanyika watu wa dini mbalimbali wanaofunga mwezi huu na wengine mwezi mwingine lakini dua ni dua kupitia kwa mwanadamu yeyote Mwenyezi Mungu inamfikia, hivyo basi tuzidi kushikamana kwa kila jambo”.

Aliendelea kusema kuwa  amani inatafutwa kwa miaka mingi lakini inaweza kutoweka kwa muda mchache hivyo basi kila mtu hasa viongozi wa dini  watumie muda wao kuhubiri umuhimu wa amani katika nchi na neno amani lisitoweke  ndani ya vinywa vyao.

Kwa upande wake Sheikhe Athuman Kinyozi alimshukuru Mama Kikwete kwa futari aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema kuwa mtu anayejitoa kwa ajili ya kufuturisha wengine  anapata thawabu kwa Mwenyezi Mungu.

Sheikhe Kinyozi alisema kuwa kufanya kitendo cha kufuturisha si lazima uwe na uwezo mkubwa kifedha bali unaweza ukanunua hata tende au maji na kuwapa watu waliofunga kile ulichowapa kikiwa ni kitu cha kwanza kutia midomoni mwao utalipwa thawabu za funga ya wale wote uliowapa kitu walichokula.

No comments: