Tangazo

August 6, 2013

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

YAH: UFAFANUZI KUHUSU HABARI ILIYOANDIKWA KATIKA GAZETI LA NIPASHE LA TAREHE 05 AGOSTI, 2013 INAYOSOMEKA “ELIMU: AIBU, AIBU”

Katika gazeti la Nipashe la leo Jumatatu tarehe 5 Agosti, 2013 toleo Namba 057834 ukurasa wa mbele na wa nne kuna habari inayosomeka “Elimu: Aibu, aibu”. Katika habari hii mwandishi anaelezea kwamba kuna Madudu zaidi yamebainika katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, baada ya kuwapanga baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano kwenye shule ambazo hazina masomo ya michepuo yao.

Habari hiyo imenukuliwa kimakosa kutoka katika Tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo imepotosha ukweli wa Taarifa husika. Usahihi wa Taarifa yenyewe ni kwamba wanafunzi waliobadilishiwa shule ni wale walioomba wenyewe kubadilishiwa michepuo (combination) na si kwamba walibadilishwa kutokana na kukosa michepuo waliyopangiwa awali katika shule hizo.

Aidha, wanafunzi wengine waliobadilishiwa shule ni wale waliopangwa mbali kutoka sehemu wanazoishi, walio wagonjwa wanaohitaji kuwa karibu na hospitali na walioomba kupangwa katika shule za kutwa kutokana na sababu za kiuchumi.

Wizara huwapanga wanafunzi wa Kidato cha tano kwa kufuata Taarifa zilizojazwa na wanafunzi wenyewe kwenye Selection Form (SEL Form) ambapo wanafunzi wanajaza machaguo yao kulingana na matarajio yao.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitangaza matokeo ya kupangwa Kidato cha 5 wanafunzi waliohitimu kidato cha 4 mwaka 2012 tarehe 10 Julai, 2013. Baada ya tangazo hilo, Wizara ilipokea maombi ya wanafunzi wanaotaka kubadili shule au machaguo (combinations) walizopangwa kwa sababu mbalimbali. Wizara ilitafakari maombi hayo na kufanya mabadiliko ya shule/ machaguo.

Imetolewa na:
Ntambi Bunyazu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
 05/08/2013

No comments: