Tangazo

August 14, 2013

WAJUMBE WA KAMATI ZA HESABU ZA SERIKALI WATAKIWA KUWA WAADILIFU

Spika wa Bunge, Mama Anna Makinda
Na Veronica Kazimoto – MAELEZO
Bagamoyo

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amewataka wajumbe wa Kamati za Hesabu za Serikali kuwa waadilifu katika utendaji wao wa kazi ili fedha zinazotengwa kwenye Bajeti zitumike ipasavyo katika kuleta maendeleo na hatimaye kumnufaisha kila mwananchi.

 Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wiki moja ya kamati zinazohusika na hesabu za Serikali wilayani Bagamoyo, Makinda amesema wabunge ndio tegemeo kubwa la wananchi hivyo ni lazima wafanye kazi zao kwa ufanisi na uadilifu mkubwa ili kuwanufaisha wapiga kura wao.

“Hili neno bahasha, bahasha lisiwepo kabisa katika utendaji kazi wa wabunge, na ni lazima wajumbe mkumbuke kuwa ninyi wabunge ndio tegemeo la wananchi katika kusimamia ipasavyo fedha za Serikali”, amesisitiza Makinda.

Amewashauri wajumbe wa kamati hizo kufuatilia kwa makini matumizi ya fedha za Serikali kwenye ofisi za wizara, idara, taasisi, na mashirika muhimu ya Serikali ili ofisi hizo ziwe mfano kwa zingine.

Kamati zinazopewa mafunzo hayo ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati mpya ya Bajeti ambazo pamoja na mambo mengine zina jukumu la kusimamia uhalali wa matumizi ya bajeti kwa kukagua kama fedha za Serikali zimetumika kama zilivyokusudiwa.

Anne Makinda amewaambia wajumbe wa kamati hizo kutumia fursa ya mafunzo hayo kujifunza kwa makini kwa kuwa ukaguzi wa fedha unahitaji utalaamu ambao utawasaidia kufanya kazi yao kwa ufanisi.

Baadhi ya mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na nafasi ya Bunge katika kusimamia matumizi na mapato ya Serikali, mbinu mbalimbali zinazotumika kutathmini uhalisia wa matumizi ya fadha za umma, uhusiano wa Bunge na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na uendeshaji wa vikao vya kamati za uwajibikaji.

No comments: