Na Veronica
Kazimoto – Dar es salaam
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2013 umepungua hadi kufikia
asilimia 6.7 kutoka asilimia 7.5 za mwezi Julai, 2013 kutokana na kupungua kwa
bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Akitoa taarifa
kwa waandishi wa habari kuhusu mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Agosti 2013
leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Ephraim
Kwesigabo mesema kupungua kwa
mfumuko wa Bei nchini kumechangiwa na kupungua kwa bei za Bidhaa za Vyakula na Vinywaji
Baridi kutoka asilimia 8.0 kwa mwezi Julai, 2013 hadi asilimia 6.5 za mwezi
Agosti, 2013.
Kwesigabo amefafanua kuwa kasi ya ongezeko la bei kwa bidhaa zisizo za
vyakula imebaki kuwa asilimia 7.3 kwa mwezi Agosti, 2013 kama ilivyokuwa mwezi
Julai, 2013.
“Kupungua kwa Mfumuko wa Bei kunamaanisha kuwa, kuna unafuu wa maisha
kwa mlaji; kwa maana hiyo Tanzania inaonyesha kuwa inapiga hatua nzuri katika
uchumi wa nchi yetu”, amesema Kwesigabo.
Amezitaja bidhaa
za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kuwa ni pamoja na mikate
na nafaka (asilimia 2.2), vitafunwa (asilimia 3.8), mahindi (asilimia 1.6),
unga wa ngano (asilimia 2.5), unga wa muhogo (asilimia 0.6), mtama (asilimia 3.4)
na kuku wa kienyeji (asilimia 0.9).
Bidhaa nyingine
ni samaki wabichi (asilimia 2.6), karanga (asilimia 2.0), mbogamboga (asilimia
2.4), nyanya (asilimia 9.9), vitunguu maji (asilimia 2.0), viazi vitamu
(asilimia 4.8), mihogo (asilimia 4.1) na sukari (asilimia 0.5).
Bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kupungua
kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na; viatu (asilimia 0.3), samani (asilimia 0.1),
vyombo vya udongo (asilimia 1.0), na vifaa vya elekroniki vya kurekodia picha
na sauti (asilimia 0.3).
Wakati huohuo Mkurugenzi Kwesigabo amesema kuwa
thamani ya shilingi ya Tanzania
kwa mwezi agosti, 2013 imepanda ikilinganishwa na mwezi septemba 2010.
Akitolea mfano wa shilingi 100, Kwesigabo
amefafanua kuwa uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na
huduma umepungua hadi kufikia Shilingi
71 na Senti 46 kwa mwezi Agosti 2013.
“Hii inamaanisha kuwa,
ili Mlaji aweze kununua bidhaa na huduma sawa na alizokuwa akinunua kwa
Shillingi 100 mwezi Septemba, 2010 atahitaji Shilingi 28 na Senti 54 zaidi,
yaani awe na Shilingi 128 na Senti 54 mwezi Agosti, 2013”, amesema Kwesigabo.
Mfumuko wa Bei nchini
umeanza kuonyesha mwelekeo unaofanana na nchi jirani za Afrika mashariki
hususani Kenya na Uganda .
No comments:
Post a Comment