**********************
Baada ya ukimya wa muda mrefu, Malkia wa Zouk
Tanzania, Hafsa Kazinja, anaibuka upya katika fani akiwa na
ingizo lake la kwanza kati ya kumi aliyoandaa kwa kuimba wimbo maarufu wa
NUTA Jazz Band uitwao “NIMUOKOE NANI” anauouleta hewani katika mahadhi ya
Zouk.
Hafsa Kazinja anasema ameamua kurudi ulingoni kwa kutoa wimbo
huo ili kumuenzi Mzee Muhidin Maalim Gurumo ambaye amestaafu rasmi fani ya
muziki baada ya kufanya kazi hiyo akiwa na bendi mbalimbali tokea mwaka wa
1960.
“Nimeamua kuimba wimbo huu wa “NIMUOKOE NANI” ili kumuenzi
gwiji huyu wa muziki kwani wakati yeye anastaafu na mimi ndiyo naibuka upya
baada ya kukaa kimya kwa muda”, anasema Hafsa ambaye alitoka kwa wimbo wake wa
“PRESHA” aliomshirikisha Banana Zorro.
Hafsa ameandaa wimbo huo wa “NIMUOKOE NANI” katika studio za OM
Productions ya jijini Dar es salaam chini ya wanamuziki nguli, Abdul Salvador
na Omari Mkali.
“Nafurahi kwamba wimbo wa NIMUOKOE NANI nimeuimba baada ya
kupata Baraka zote toka kwa mtunzi na mwimbaji wake Mzee Gurumo mwenyewe.
“Haikuwa rahisi kama inavyoweza kudhaniwa kwani baada ya kwenda
kumuona nyumbani kwake alinifanyisha mtihani wa kuuimba wote kabla ya kuridhika
maana alisema asingefurahi kuona wimbo wake unaimbwa hovyo hovyo na kuharibiwa
radha yake”, anasema Hafsa, ambaye hivi sana
anamalizia ngoma zake zingine tisa alizotunga mwenyewe, kabla ya kuvamia anga
kwa mara ingine.
Hafsa anasema katika ukimya wake amekuwa akifanya utafiti na
kujifunza kwa undani zaidi fani ya muziki, akipata mawaidha maridhawa toka kwa
wanamuziki nguli ndani nan je ya nchi wakiwemo Muhidin Maalim Gurumo, Omar
Mkali, Abdul Salvador na Lokassa ya Mbongo wa Congo aliyekutana na kufanya naye
kazi alipokuwa ziarani Marekani hivi karibuni.
Msanii huyu wa kizazi kipya anasema ataitambulisha rasmi ngoma
ya “NIMUOKOE NANI” katika tamasha la kumuenzi Mzee Gurumo lililopangwa
kufanyika OKtoba 1, 2013 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam .
“Natumaini wapenzi wa muziki watafurika kwa wingi kwenye tamasha
hilo name
naahidi kuitendea haki ngoma ya “NIMUOKOE NANI” hivyo wasikose kuja kujionea
wenyewe jinsi sie wa kizazi kipya tunavyoweza kufanya kazi na wakubwa wetu wa
kazi, anaongezea Hafsa ambaye pia anaandaa video yake pamoja na ya ngoma zake
zingine mpya.
Mkongwe Abdul Salvador, ambaye alikuwa mmoja wa waanzilishi
wa bendi ya TANCUT ALMASI YA Iringa iliyotamba na mtindo wake wa “FIMBO
LUGODA”, anamtaja Hafsa kazinja mmoja wa wanamuziki wa kike waliojaaliwa sauti
nzuri na kipaji cha hali ya juu hapa nchini.
“Kwa kuweza kuimba wimbo wa Mzee Gurumo na kupatia kisawasawa
inadhihirisha kwamba Hafsa ni mwanamuziki aliyekomaa maana si mchezo kuimba
nyimbo ya wakongwe kwa ufasaha kama
alivyofanya Hafsa.
“Na hii inadhihirisha kwamba uwezekano wa kizazi kipya na cha
zamani kufanya kazi pamoja ni mkubwa sana na
sioni kwa nini isiwe hivyo”, anasema Salvador .
Omari Mkali, aliyetamba na bendi ya CHUCHU SOUNDS, chini ya
marehemu Yusuf Chuchu, naye anamwelezea Hafsa Kazinja kama moja ya majembe ya
muziki hapa nchini kwa upande wa kinamama, na kwamba anaweza kufika mbali
endapo kama moto aliokuja nao upya
atauendeleza.
IMETOLEWA NA
OM PRODUCTIONS NA HISIA SOUNDS
No comments:
Post a Comment