Tangazo

October 7, 2013

CPC CHA CHINA WAWASILI KUSHIRIKI MKUTANO WA MAKATIBU WAKUU WA VYAMA VYA UKOMBOZI KUSINI MWA AFRIKA

 Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Dk.Asha-Rose Migiro akimkaribisha Naibu Waziri katika Idara ya Kimataifa ya Chama Cha Kikomunisti cha China Ai Ping ambaye amewasili nchi   kuhudhuria Mkutano wa Sita wa Vyama Vya Ukombozi Afrika utakaofanyika tarehe 9 Oktoba 2013 Kunduchi mjini Dar es salaam.
Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa  Dk.Asha-Rose Migiro akizungumza na Naibu Waziri katika  Idara ya Kimataifa ya Chama Cha Kikomunisti Ai Ping mara tu alipowasili nchini kwa kuhudhuria mkutano wa sita wa Vyama vya Ukombozi.
 XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Leo Jumatatu tarehe 07/10/2013 Chama cha Mapinduzi kinapokea ugeni mkubwa wa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika. Makatibu Wakuu hawa wanakuja kuhudhuria Mkutano wa Sita ambao ni mwendelezo wa mikutano ya aina hii inayofanyika mara mbili kwa mwaka.


Vyama vyote vya Ukombozi vitahudhuria Mkutano huu utakaofanyika  jijini Dar es Salaam tarehe 09 Oktoba.  Vyama hivyo ni ANC cha Afrika ya Kusini; FRELIMO cha Msumbiji, MPLA cha Angola; SWAPO cha Namibia; ZANU-PF cha Zimbabwe na Chama mwenyeji CCM.

Mkutano wa Makatibu Wakuu utatanguliwa na mikutano ya Jumuiya za Vijana, Wanawake na Maveterani itakayofanyika Jumanne Oktoba 8, 2013.

Mkutano wa Sita wa Makatibu Wakuu utahudhuriwa pia na  ujumbe kutoka Chama rafiki cha Kikomunisti cha China utakaoongozwa na Ndugu Ai Ping, ambaye ni Naibu Waziri anayeshughulikia Idara ya Kimataifa ya Chama hicho.

Pamoja na mambo mengine Mkutano huu wa Sita wa Makatibu Wakuu wa vyama vya Ukombozi kusini mwa Afrika utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa katika kikao chao cha tano kilichofanyika huko Tshwane, Afrika ya Kusini mwezi Machi, 2013.

Mojawapo ya maazimio hayo ni ujenzi wa Chuo cha Pamoja cha Vyama hivi vya Ukombozi utakaofanyika Ihemi, katika mkoa wa Iringa. Makatibu Wakuu wanatarajiwa kuzuru eneo la Ihemi tarehe 08/10/2013 kama sehemu ya maandalizi ya majadiliano ya Mkutano huo wa Sita.

Mkutano huu  utafunguliwa  rasmi na Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi tarehe 09/10/2013.

 Imetolewa na :-

Asha-Rose Migiro
KATIBU WA SIASA NA UHUSIANO WA KIMATAIFA
CHAMA CHA MAPINDUZI
07/10/2013
 

No comments: