Tangazo

October 7, 2013

DK MWINYI: JAMII INA UELEWA MDOGO WA TATIZO LA AFYA YA AKILI

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi.
 NA MAGRETH KINABO – MAELEZO

 IMEELEZWA kuwa uelewa mdogo wa jamii kuhusiana na matatizo mbalimbali ya afya ya akili kwa wazee ndicho chanzo cha idadi ndogo ya mahudhurio  katika vituo vya kutolea  huduma  za afya nchini.

 Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii. Dk. Hussein Mwinyi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dares Salaam kuhusu siku ya Afya ya Akili  Duniani itakayoadhimishwa  Oktoba 10, mwaka  huu.

 Dk. Mwinyi  alisema kutokana na taarifa  ya afya na magonjwa  ya  akili   ya mwaka 2012/2013 inaonesha kuwa takribani  wazee 13,789 wameweza kuhudhuria  kwenye  vituo  vya  kutolea  huduma ya afya nchini.

Aliongeza kwamba takwimu  zinaonesha kuwa Tanzania  ina wazee takribani milioni  2.56 na inakadriwa kuwa ifikapo mwaka 2050  wazee watakuwa asilimia 10 ya Watanzania wote.

“ Hii inaonesha kuwa tatizo la afya  ya akili kwa wazee nalo litaongezeka,”alisema Dk. Mwinyi huku akiongeza kuwa kutokana na takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa kuwa na asilimia saba ya wazee wote nchini na mkoa wa Tanga unashika nafasi ya sita yenye asilimia 4.8 ya wazee wote nchini.

 Aliongeza kuwa kila mtu anatakiwa kuhakikisha anatoa msaada wa kutosha kwa wazee, ikiwa ni pamoja na kupunguza unyanyasaji. Pia ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya afya ya afya ya akili.

“ Endapo  utatambuliwa kuwa una ugonjwa huo tumia huduma za afya  kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya,” alisisitiza.

 Alivitaja visababishi ambavyo husababisha matatizo ya afya aya akili kwa wazee, kuwa ni umasikini, kutengwa na jamii, kufiwa na mtu wa karibu, kupoteza mali, kupoteza kazi au kuwa mlemavu kukosa huduma muhimu, unyanyapaa, unyanyasaji na ubaguzi.

 Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa hayo Kissa Mwabene alisema changamoto wanayokabiliana nayo katika utoaji wa huduma hiyo ni ukosefu wa dawa za kutosha, Akijibu swali hilo Dk. Mwinyi  aliwataka watoa huduma hiyo  kupeleka  maombi mahali husika  ya ili  waweze kupatiwa  huduma hizo.

  Aidha taaluma hiyo inakabiliwa na wataalamu wa kutosha , kwa mujibu wa  Dk. Fausta Philip ambaye ni mtaalamu wa magonjwa hayo.

Akijibu hoja Waziri huyo alisema sekta ya afya inakabiliwa na upungufu wa wataalamu kwa asili 43 katika  nyanja zote, hivyo Serikali itaendelea kuongeza udahili  ili kukidhi haja ya huduma  za afya  ikiwemo  taaluma hiyo.  

No comments: