Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WADAU watano, ikiwamo Kampuni ya usafirishaji ya Phed Trans
inayomilikiwa na mdau wa muziki na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf
Mhandeni, maarufu kama (Yusuphed Mhandeni), wamejitokeza kudhamini Tamasha la
Utamaduni linalotarajiwa kufanyika Handeni mjini, mkoani Tanga, Desemba 14
mwaka huu.
Mratibu wa Tamasha la Utamaduni Handeni, mkoani Tanga.
Wengine waliokubali kuwezesha tamasha hilo kwa namna moja
ama nyingine ni Katomu Solar Specialist, Business Country Director (BCD) duka
la mavazi la Chichi Local War, SmartMind
& Partners ambayo ipo chini ya ANESA COMPANY LIMITED, ambapo
katika tamasha hili, watadhamini kwa kupitia kitabu cha ‘NI WAKATI WAKO WA KUNG'AA’,
kilichoandikwa na Albert Nyaluke Sanga, bila kusahau kampuni ya utengenezaji
matangazo ya Screen Masters ambapo pia inamiliki mtandao wa Saluti5.com, ikiwa chini ya Mkurugenzi wake Said Mdoe.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Tamasha
hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa wadau hao ndio wa kwanza kujitokeza kuwezesha
kwa tukio hilo, huku mazungumzo yakiendelea kwa wengine wenye nia ya kudhamini
tamasha hilo.
Alisema ishara njema imeanza kujitokeza kuwa wadau na
makampuni mengi zaidi yanaweza kuingia kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tamasha
hilo linafanyika kwa mara ya kwanza na kuweka historia katika harakati za
kukuza utamaduni kama ishara ya kuleta maendeleo.
“Tunashukuru kwa kampuni hizi kuwa za kwanza kuthibitisha
kushiriki na sisi kwa namna moja ama nyingine juu ya kufanyika kwa tamasha
hili, hivyo naamini kwa pamoja tutafanikisha na kuwezesha kufanya kile
tunachokusudia.
“Bado juhudi zinafanyika kuingia kwa wadhamini wengi zaidi
ikiwa ni njia ya ushirikiano kati yetu sambamba na wadau hao kuwa na nafasi
kubwa ya kutangaza biashara zao kwa Watanzania wote, hususan wakazi na wananchi
wa Handeni kwa ujumla wake,” alisema Mbwana.
Aidha, Mbwana alitumia fursa hiyo kuwashukuru walioanza
kujitokeza kudhamini tamasha hilo na kuzitakaka kampuni, taasisi, mashirika
mbalimbali pamoja na watu binafsi wenye nia ya kukuza na kuthamini utamaduni
wajitokeze ili kuhakikisha kuwa Tamasha hilo linafanyika kwa mguso na kufikisha
kile kilichokusudiwa kwa hadhira.
Tamasha hilo limeanza kugusa hisia za watu wengi kutokana na
kuwa na mipango thabiti ya kulifanya kwa mafanikio, ikiwa ni njia pia ya
kuwakutanisha wananchi kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kufikiria mambo ya
kimaendeleo, huku likiandaliwa na Raha Company and Entertainment.
No comments:
Post a Comment