Tangazo

February 7, 2014

KAMISHNA WA SENSA ATOA SOMO KWA WADADISI NA WAHARIRI WA MADODOSO YA UTAFITI WATU WENYE UWEZO WA KUFANYA KAZI 2014

Wadadisi na Wahariri wa madodoso ya watu wenye uwezo wa kufanya Kazi kutoka mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara wakiwa  kwenye mafunzo ya siku  mjini Morogoro.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na. Veronica Kazimoto na Aron Msigwa – Morogoro.

Wadadisi na Wahariri wa madodoso ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi  mwaka 2014 wametakiwa kuzingatia maadili na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuepuka kuliletea taifa hasara  kwa kutoa takwimu zisizosahihi.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Morogoro na Kamishna wa Sensa ya Watu na   Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said wakati akizungumza  na Wadadisi na Wahariri wa madodoso yaUtafiti wa Watu wenye uwezo wa kufanya kazi kutoka mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara walio katika mafunzo ya siku 16 mjini Morogoro.

 Amesema  ili majibu ya takwimu zinazokusanywa yawe sahihi ni lazima wataalam hao wazingatie kanuni na taratibu zilizowekwa katika kupata uhalisia wa taarifa za watu za eneo husika badala ya kutoa takwimu zisizo sahihi.

“Tunachotegemea kutoka kwenu ni kwamba mtakayojifunza na kuyafanya kwa vitendo hapa  mtakwenda kuyafanyia kazi na kutuletea takwimu sahihi na sio za kupika mtaani, na kuepuka kuzungumza na watu wachache wa kikundi Fulani kuwakilisha maeneo yote” Amesisitiza.

Amesema kuwa yapo mambo mengi ya kuzingatia ambayo wao kama wadadidisi na wahariri wanapaswa kuyafuatilia wakati wa ukusanyaji wa takwimu hizo ikiwemo idadi ya watu wenye umri wa kwenda shule ambao bado wako nyumbani ili  kuisaidia serikali kupanga mipango ya maendeleo.

Ameongeza kuwa ukusanyaji wa takwimu hizo ni muhimu kwa sababu zinaondoa utata katika kushughulikia changamoto mbalimbali katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwepo wa usahihi wa taarifa kuhusu makundi ya watu na kazi zao, kipato,masomo, uwezo wa kufanya kazi na utegemezi  na kuondoa tatizo la baadhi ya taasisi kutumia takwimu zisizo sahihi kujipatia fedha isivyo halali kwa mambo yasiyokuwepo.

Akitoa ufafanuzi wa takwimu zilizopo nchini kutokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Bi. Hajjat amesema kuwa kiwango cha ongezeko la idadi ya watu kutoka sensa ya mwaka 2002 mpaka 2012 ni asilimia 2.7 kwa maana ya ongezeko la watu milioni 10 ndani ya miaka 10 na kufafanua kuwa ni sawa na ongezeko la watu milioni 1 kila mwaka ni kubwa ikilinganishwa na hali ya uchumi uliopo.

Kuhusu mikoa ambayo wawakilishi wake wako katika mafuzo amesema kuwa mkoa wa  Morogoro idadi ya watu imeongezeka kwa asilimia  2.4, mkoa wa Pwani asilimia 2.2, Dar es salaam 5.6 ongezeko ambalo ni kubwa sana.

“Hii ni changamoto kubwa sana kwa mkoa wa Dar es salaam na ipo haja ya kuchukua hatua kwa sababu kila kilometa moja ya mraba wanaishi watu 3133 hata sehemu ya kumwaga taka na sehemu ya kupitisha maji inakuwa tatizo kutokana na msongamano wa watu’’ amesisitiza.

Aidha katika mkoa wa mkoa wa Lindi idadi ya watu imeongezeka kwa asilimia 0.9, Mtwara ikifikia asilimia 1.2 na kuongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa idadi hiyo kuongezeka zaidi kutokana na ugunduzi wa gesi na mafuta katika  mkoa wa Mtwara ongezeko la watu katika mkoa huo litakuwa kubwa kutokana na uwekezaji mkubwa katika mkoa huo.

No comments: