Na Mwandishi maalumu - HakiElimu
Uchunguzi kuhusiana na vitabu vilivyonunuliwa
kutokana na chenji ya rada na kusambazwa mashuleni nchini Tanzania umebaini
kuwa vitabu hivyo vina kasoro za ubora licha ya kupata Hati ya Ithibati
(Certificate of Approval) kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi.
Uchunguzi huo uliofanyika katika shule za
msingi katika Wilaya ya Kilwa Masoko iliyoko mkoani Lindi umebaini pamoja na
kasoro za ubora pia mgawanyo wa vitabu hivyo haukuzingatia mahitaji halisi kwa
shule husika. Hii imesababisha upotevu wa pesa za Watanzania zilizorudishwa
nchini baada ya kuokolewa katika ufisadi wa manunuzi ya rada.
MAPUNGUFU KATIKA VITABU VYA SOMO LA SAYANSI
Mwalimu mmoja wa somo la Hisabati (jina
linahifadhiwa) anayefundisha darasa la saba ameelezea kupokea vitabu vya kiada
vinavyokinzana katika mada akitolea mfano wa mada ya “Ubongo wa Nyuma,” ambapo
kitabu cha mchapishaji mmoja kikiandika kuwa Serebelamu huhusika na matendo yasiyo
ya hiari huku kitabu kingine kikielezea Serebelamu huhusika na uratibu
wa matendo ya hiari. Picha ifuatayo inaonesha mkanganyiko uliopo katika
mada ya “Aina za Misuli” ambapo wachapishaji wanataja majina na aina tofauti za
misuli.
MAPUNGUFU KATIKA VITABU VYA SOMO LA
KISWAHILI
Akizungumzia baadhi ya kasoro katika kitabu cha
somo lake, mwalimu wa somo la Kiswahili darasa la sita amesema moja ya kasoro
katika kitabu kilichopokelewa ni kutokuwa na mtiririko maalum wa mada na kuleta
mkanganyiko kwa wanafunzi na walimu. Video ifuatayo inaonesha jinsi mada ya
“Aina za Maneno” ilivyowasilishwa katika kurasa katika ukurasa wa 10, 85 na 118
katika kitabu kimoja, Gonga hapa kuitazama http://bit.ly/1suMuSq
MAPUNGUFU KATIKA SOMO LA HISABATI
Mwalimu wa Hisabati aliyepata nafasi ya
kushiriki katika utafiti huu amezungumzia kuwepo mazoezi machache sana na
mepesi yasiyoweza kumpa mwanafunzi uwezo wa kutafakari na kupambanua.
Vile vile vitabu hivyo vinasemekana kutokuwa na majibu sahihi ya maswali
yaliyotolewa na hivyo kuwapotosha wanafunzi. Picha ifuatayo inaonesha jibu
ambalo halikukotolewa mpaka mwisho na hivyo kutoa jibu lisilo sahihi katika
taaluma ya Hisabati.
|
MAPUNGUFU KATIKA SOMO LA JOGRAFIA
Katika somo la Jiografia , baadhi ya makosa
yaliyogundulika ni pamoja na kuwepo kwa taarifa zinazopotosha wanafunzi; mfano
katika mada ya “Majira ya Dunia “katika kitabu kimoja cha kiada kilichonunuliwa
kwa chenji ya rada kina makosa katika tarehe za kupatwa kwa jua kama
inavyoonekana pichani.
MATUMIZI MABAYA YA RASILIMALI ZA UMMA
Utafiti uliofanywa katika shule nne (4)
umegundua kuwa licha ya Serikali kuwa na takwimu za mahitaji halisi ya vitabu
vya shule hizo kulingana na masomo, mgawanyo wa vitabu vya chenji ya rada bado
una mapungufu makubwa.
Masomo ambayo yalikuwa yana upungufu mkubwa wa vitabu
bado yameendelea kutopata kabisa kitabu hata kimoja na au kupokea nakala
chache huku masomo mengine yakipokea vitabu vingi mpaka kupitiliza
mahitaji halisi ya shule husika. Masomo ambayo yameendelea kukabiliwa na
upungufu wa vitabu kwa upande wa Wilaya ya Kilwa ni pamoja na Uraia, Haiba na
Michezo, Stadi za kazi na Historia .
No comments:
Post a Comment