Tangazo

August 21, 2014

MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA AUNDA KAMATI NDOGO

Na Magreth Kinabo, Dodoma  

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta (pichani),ameunda kamati ndogo yenye ujumbe wa watu 10 kwa ajili ya kushughulikia masuala ambayo  hayakufikia muafaka wakati wa majadiliano ya kupitia sura mbalimbali za Rasimu ya Katiba Mpya kwenye Kamati 12 za Bunge hilo.

Kamati hiyo itakuwa inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Samia Suluhu Hassan,ambapo  wajumbe  wa kamati hiyo wametoka kila pande ya Muungano  yaani watano wametoka Tanzania Bara na watano kutoka Zanzibar. 

Aidha Mhe. Sitta akizungumzia kuhusu  maendeleo  ya kazi za Kamati hizo, ambapo alisema zinaendele vizuri, hivyo kuanzia wiki ijayo sura zote 15 zitakuwa zimepigiwa kura,hivyo  Kamati hizo zitakuwa zimemaliza sura 17 ya rasimu hiyo na za nyongeza ifikapo Agosti 27,mwaka huu  ili kuanza kuwasilisha katika Bunge hilo kuanzia Septemba 2,mwaka huu.

Hayo yalisemwa leo na  Mhe. Samuel Sitta wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokutana nao leo kuhusu muhtasari wa kikao cha Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo kilichokaa leo kutathmini kazi za Kamati 12 za Bunge hilo lilipofikia pamoja kuridhia baadhi ya mapendekezo ya kuongeza Ibara na sura ndani Rasimu ya Katiba katika Kamati zao. 

Mwenyekiti huyo aliyataja mambo ambayo yatashughulikiwa na kamati hiyo, ni muundo wa  Bunge  katika masuala  ya Muungano, uraia pacha, mahakama ya kadhi na kamati ya pamoja ya fedha.
“Haya mambo manne nimeagiza ufanyike utaratibu maalum,” alisema Mhe. Sitta.  

 Mhe . Sitta  akizungumzia kuhusu tathimini ya mwenendo wa Kamati hizo, alisema zipendekeza masuala kadhaa na kuacha mengine  kama yalivyo katika rasimu hiyo.  

Akizungumzia kuhusu yaliyojadiliwa katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo,kabla ya kukutana na waandishi wa habari, Mhe. Sitta alisema kamati hiyo imepokea mapendekezo kutoka katika kamati mbalimbali kuhusu kuongezeka kwa sura na Ibara za rasimu hiyo.

Aliyataja mapendekezo hayo , likiwemo la  Tume ya Marekebisho ya Katiba lililowasilisha na Jaji Warioba kuhusu ardhi, mazingira na rasilimali za taifa, Jumuia ya Tawala  za  Serikali za Mitaa (ALAT) na pendekezo la Haki ya Watumiaji huduma na bidhaa ili kuwalinda walaji lililowasilishwa , Hawa Ng’umbi  ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo.

Aliyataja  mapendekezo  mengine  ni la  Jukumu la Serikali kujenga uchumi imara, ambapo lengo ni kuwa na maendeleo ya uchumi wa ujamaa na kujitegemea na Kuwepo kwa Baraza la Habari, la wajumbe wa 201 kuhusu ardhi, wafugaji, wavuvi pia na wachimbaji wadogo ili ziweze kutungwa Sheria za kusimamia masuala hayo. 
 
Mhe. Sitta  alisema kutokana na mapendekezo  hayo kutakuwepo na ongezeko la ukurasa na sura kadhaa katika rasimu hiyo. 

Alisema Kamati imebaini tatizo la mahudhurio,  aliwapongeza wajumbe wa Bunge hilo kutoka upande wa Zanzibar kwa kuwa na mahudhurio mazuri kwenye vikao kuliko kutoka  Tanzania Bara kuacha visingizio vya kutohudhuria vikao.

Katika hatua nyingine Mhe. Sitta alisema kutakuwepo na wataalamu kabla ua kumalizika  kwa wiki hii kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa kutoka Hazina kwa pande zote za Muungano, ambapo ataukuwepo pia Gavana wa Benki Kuu, Profesa Bonaventure Rutinwa kwa ajili ya suala la uraia pacha, uhamiaji  na Profesa Issa Shivji ambaye ataoa ufafanuzi juu ya aina ya Muungano ili kuwa na uwiano kwa kuwa hivi sasa yapo mambo machache.

No comments: