Tangazo

September 15, 2014

SERIKALI YASEMA BUNGE MAALUM LA KATIBA LINA UHALALI KISHERIA NA KISIASA KUENDELEA

Na Magreth Kinabo,Dodoma 
Serikali imesema kwamba Bunge Maalum la Katiba linaendelea kwa mujibu wa Sheria, mjadala wa hoja ya kusitishwa kwa Bunge hilo, umefungwa rasmi leo.

Aidha Serikali imewaondoa hofu wananchi kwamba hakuna mgogoro wa kisiasa, hivyo waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato(riziki) kama kawaida, pia ipo macho kupitia vyombo vyake vya usalama,itasimamia sheria na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na amani na utulivu.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Asha  Rose  Migiro kwenye kikao cha Arobaini cha Bunge hilo wakati akitoa tamko la Serikali  kwenye mjadala wa mwisho wa kujadili sura zote 15 zilizobakia za Rasimu ya Katiba Mpya.

“Bunge hili linaweza kuendelea na shughuli zake. Nawaomba Watanzania wafahamu mjadala wa kusitisha Bunge umehitimishwa hii leo kisheria na Mahakama Kuu ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Dk. Migiro.

Dk. Migiro aliongeza kuwa  kwa taarifa walizonazo majadiliano baina na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania(TCD) pamoja na vyama vyote husika yataendelea Septemba 17 na 18, mwaka huu, kwa sababu mchakato huo si wa chama kimoja, wala viwili au vitatu , bali  mchakato wa Watanzania wote kupitia mfumo ambao umewekwa  wa vyama vyote kisheria.

Akizungumzia kuhusu takwimu za wajumbe wa Bunge hilo, Dkt. Migiro alisema  kuwa lina wajumbe 630, kati yao waliotoka nje ya Bunge hilo ni wajumbe 130 ni sawa na asilimia 21 ya wajumbe wote.

“Wajumbe waliobakia ndani ya Bunge hili ni 500, sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote, tukitazama mambo ya takwimu kwa  kutambua Kundi la 201. Imejitokeza dhana kwamba wajumbe waliobakia humu ndani ni wa aina moja, hiyo si kweli,”alisema.

Dk. Migiro alisema  kati ya wajumbe 500, waliobaki katika Bunge hilo, 189, wanatoka katika kundi la 201.

Alisema wajumbe  wengine waliobakia, 348 wanatoka upande wa Tanzania Bara, kati ya hao, wajumbe 125 ni wajumbe wanaotoka Kundi la 201.

“ Tukiangalia upande wa Zanzibar wajumbe waliobakia ni 152, kati yao wajumbe 64 wanatoka Kundi la 201.Tungependa kusisitiza Kundi la 201 ndio wajumbe ambao kwa wingi wao kitakwimu na kimakundi wanawakilisha Taifa  letu  kwa sura zote.

“ Ni dhahiri waliobakia humu ndani ni wengi, hii ina maana kwamba kwa kuzingatia matakwa ya masuala ya kisheria kwa maridhiano, kwa majadialiano na kwa kushawishi hoja. 

“Wajumbe waliobakia  ni wengi wana uhalali kisheria na kisiasa. Tutaendelea na shughuli zetu kama sheria inavyotutaka, uwakilishi wa Bunge umetimia …  tuna wajibu  wa kisheria wa kufanya yale tunayoyataka kuyafanya,” alisisitiza  huku akisema waliotoka nje  kwa pande zote mbili hawafikii theluthi moja.

Alifafanua kuwa vyama vilivyotoka nje ya Bunge hilo, ni vitatu,vilivyobakia  ndani ya ni 18 ambavyo vimesimamia na vinaendelea kusimamia umoja wa kitaifa  wa nchi yetu. 

Akichangia mara baada ya tamko hilo, mjumbe wa Bunge hilo, John Shibuda alimpongeza mtoa taarifa hiyo ya Serikali na kuipongeza Serikali kwa kushinda kesi.
Aliwataka Watanzania kuchuja kati ya siasa na maslahi binafsi.

No comments: