Tangazo

September 12, 2014

WAGONJWA WA SARATANI WAIOMBA SERIKALI IWEZE KUTOA HUDUMA YA MATIBABU KATIKA HOSPITALI NYINGI ZAIDI

Anna Nkinda – Maelezo

Serikali imeombwa kuangalia uwezekano wa kutoa huduma ya matibabu ya ugonjwa wa saratani za wanawake  kwenye Hospitali zingine nchini kwani hivi sasa huduma hiyo inatolewa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pekee.

Ombi hilo limetolewa leo na wanawake wanaokabiliwa  na tatizo la ugonjwa wa saratani ya mlango wa  kizazi na matiti wakati wakiongea na  waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa siku tatu wa saratani za wanawake unaofanyika katika Hoteli ya Court Yard jijini Dar es Salaam.

Wanawake hao walisema inachukua muda mrefu pale ambapo utagundulika una ugonjwa wa saratani hadi kupata matibabu lakini kama huduma hiyo itatolewa katika Hospitali zingine itarahisisha kwa mgonjwa kupata matibabu kwa wakati.

Mmoja wa wanawake  anasumbuliwa na saratani ya titi alisema wanawake wengi wanafikiria ukiugua saratani unakwenda kufa jambo ambalo siyo kweli kwani yeye ameishi na ugonjwa huo kwa muda wa miaka 16 sasa.

“Nawashauri wanawake wenzangu waende kufanya vipimo vya mara kwa mara kwani kuna vipimo ambavyo ukipima utajua kama unatatizo  au la na kama utakutwa  na ugonjwa  utapata dawa mapema”, alisema mgonjwa huyo.

Naye mmoja wa wanawake  anayeumwa ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi alisema dalili ya kwanza aliyoiona ni kutokwa na damu ukeni akaamua kwenda kufanya vipimo na baada ya kukutwa na tatizo akapata matibabu katika Taasisi ya Saratani ya  Ocean Road.

“Nawashauri wanawake wenzangu wakiona dalili za ugonjwa huu wasikae kimya na kujidanganya kwa kutumia dawa za miti shamba bali wawahi Hospitali mapema ambako  watapata matibabu na kupona. Mimi nilipata tatizo la ugonjwa huo mwaka 2011 nilitibiwa na kupona”, alisema.

Kwa upande wake Dkt. Sara Maongezi ambaye ni Mkurugenzi wa uboreshaji Afya kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema Saratani ya mlango wa kizazi ni moja ya saratani inayoongoza kwa kuua wanawake wengi nchini.

Alisema  mkutano huo ambao umehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka  nchi za Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Madagasca, Rwanda na Burundi unalengo la kuwafanya wanawake waweze kuufahamu ugonjwa huo ili waweze kujikinga kwa wale ambao hawajapata na kwa walioupata waweze kuwahi mapema Hospitali kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.  

“Baada ya Mkutano huu tutatoka na maazimio ambayo tutayafanyia kazi na kuona jinsi gani tunaweza kuboresha utendaji wetu  wa kazi za kuielimisha jamii kuhusu ugonjwa huu”, alisema Dkt. Maongezi.

Dkt. Maongezi alisema, katika nchi za Afrika ya Mashariki takwimu zinaonyesha Tanzania inaongoza kuwa na wagonjwa wengi wa saratani za wanawake lakini bado hakuna ukusanyaji sahihi wa takwimu kwani wagonjwa wengi wanafia majumbani na wanaofika Hospitali kupata matibabu ni wachache.

Walengwa wa mkutano huo ni wanawake wanaoishi na saratani pamoja na Asasi zinazofanya kazi za saratani lengo lake ni kwa wadau hao kuweza kuilemisha jamii ili iweze kuchukua hatua  dhidi ya ugonjwa huo.

Mkutano huo umeandaliwa na Women’s Empowerment Cancers Advocacy Network, (WE CAN) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na wadau wengine wa Saratani.

No comments: