Tangazo

October 29, 2014

Mke wa Rais wa China aipa msaada Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama

Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Beijing, China

Mke wa Rais wa China Mama Peng Liyuan ameahidi kutoa vifaa vya shule vikiwemo vya maabara pamoja na vitabu kwa ajili ya shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama ili  wanafunzi hao waweze kusoma vizuri masomo ya sayansi.

Mama Liyuan aliitoa ahadi hiyo  jana wakati akiongea na  mke wa Rais Mama Salma Kikwete katika ukumbi maarufu wa watu (Great hall of the People) uliopo mjini Beijing.

“Nina mapenzi na Taasisi ya  WAMA, nakupongeza kwa kazi unayoifanya ukiwa Mke wa Rais ya kuwainua wanawake kiuchumi na kuwasaidia  watoto wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi ambao nao wanapata elimu sawa na watoto wengine”.

Najua kitaaluma wewe ni mwalimu na unapenda shule mwaka huu nitakuunga  mkono zaidi katika masuala ya shule,  hii itawasaidia wanafunzi kusoma vizuri. Pia nitakuwa na ushirikiano  endelevu na Taasisi ya WAMA”, alisema Mama Liyuan.

Kwa upande wake Mama Kikwete alishukuru kwa msaada huo na kusema kila kwenye maendeleo changamoto hazikosekani alizitaja changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ambazo ni  upungufu wa maabara, kutokuwepo kwa wataalamu wa maabara na walimu wa masomo ya sayansi wa kutosha.

Mama Kikwete  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema  katika upande wa elimu Serikali kwa kushirikiana na wananchi wamejitahidi kujenga shule nyingi za  Sekondari lakini  bado kuna  upungufu wa walimu wa masomo ya  sayansi , kutokuwa na maabara za kutosha, kutokuwa na vifaa vya maabara na  upungufu wa wataalamu wa maabara .

“Ninaomba  kuwe na ubadilishanaji wa ujuzi wa kazi (Exchange Program) kwa walimu wetu wa nchi hizi mbili hii itawasaidia kupata  utaalamu zaidi katika fani zao na kutoa mfano wa wataalamu wa maabara ambao wakija nchini watasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya sayansi kwa njia ya vitendo”, alisema Mama Kikwete.

Shule hiyo ambayo inamilikiwa na Taasisi ya WAMA wanafunzi  wake ni watoto wa kike  ambao ni yatima na wanaotoka  katika mazingira hatarishi  kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani iko  kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Hii ni mara ya pili kwa Mama Liyuan kuiunga mkono Taasisi ya WAMA ambapo mwaka 2013 alipotembelea nchini  alitoa Yuan milioni moja  sawasawa na shilingi milioni  250 za kitanzania na mabegi ya shule 100 kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama na vyerehani 20 kwa ajili ya Umoja wa Vikundi vya WAMA  (UVIMA).

Mama Kikwete  ameambatana na mumewe Rais Prof. Jakaya Mrisho Kikwete nchini China kwa ziara ya kikazi ya siku sita.

No comments: