Tangazo

December 30, 2014

Mama Kikwete awataka vijana kuwa na msimamo na kutokubali kutumika katika vurugu

Na Anna Nkinda – Maelezo, 
Lindi

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka vijana kuwa na msimamo na kutokubali kutumika katika vurugu zinazohatarisha amani na usalama wa nchi.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati akifungua shina la  vijana wakeleketwa la kikundi cha Zahanati Kempu lililopo Kata ya Rasibura wilaya ya Lindi mjini.

Alisema vijana wengi hawajui Historia ya nchi hivyo basi baadhi ya watu wasio na nia njema wanaitumia nafasi hiyo kuwarubuni na kuwashawishi kufanya vurugu zinarudisha nyuma maendeleo ya eneo husika.

“Msikubali  mkoa wetu wa  Lindi kuwa kichaka cha   majaribio na kutumika katika vurugu, kuweni  na  msimamo  wa kuitetea amani yetu  kwani mkifanya vurugu matatizo yanapotokea ninyi ndiyo mnaoangamia na hao waliowashawishi wanawakimbia”.

Kama atakuja mtu hapa na kuwashawishi  kwa ajili ya shughuli za maendeleo ni sawa hakuna atakayezuia tunahitaji kuwa na maendeleo katika mkoa wetu, lakini kuwashawishi ili mfanye vurugu na kuharibu vichache tulivyonavyo msikubali”, alisema Mama Kikwete.

Aidha MNEC huyo aliwasisitiza vijana kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili waweze kujiletea maendeleo yao na ya mkoa huo kwa kuwa vijana  ndiyo wanaotegemewa na ni nguvu kazi ya Taifa.
Akisoma taarifa ya kikundi hicho Hidaya Chivii ambaye ni Mtunza fedha alisema kikundi hicho kilianzishwa  tarehe 5/7/2014 kikiwa na  wanachama 23 kati ya hao wanaume ni 18 na wanawake ni watano.

Chivii alisema madhumuni ya kuanzishwa kwa kikundi hicho ambacho kinajihusisha na kazi ya kuendesha pikipiki  (bodoboda)  kwa upande wa wanaume na ususi kwa upande wa wanawake ni kujikwamua na hali ngumu ya maisha na kuweza kujiendeleza.

“Waendesha pikipiki  tunakabiliwa na changamoto ya kunyang’anywa pikipiki hasa ifikapo wakati wa uchaguzi kwani wamiliki walio wengi ni wanachama wa chama cha Wananchi (CUF)  na sisi ni wanachama wa CCM au wanatupa pikipiki zao kwa masharti magumu yakiwemo ya kukipigia kura chama chao”, alisema Chivii.

Alizitaja changamoto nyingine zinazowakabili kuwa ni  pamoja na kutokuwa na vitendea kazi vyao wenyewe na kutokupata mafunzo ya ujasiriamali.

Wakati huo huo Mama Kikwete  alifanya vikao na  viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM katika matawi ya Kilimahewa na barabara ya Kawawa  na kuwahimiza wajumbe  kuendelea  kushikamana na kuwa kitu kimoja ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Akiwa katika tawi la Kilimahewa lililopo Kata ya Mwenge aliwapokea vijana wanne kutoka chama cha Wananchi (CUF)  ambao walijiunga na CCM.

Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini yupo wilayani humo  kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.

No comments: