Tangazo

December 22, 2014

PROFESATIBAIJUKA NA DHANA YAUWAJIBIKAJI KISIASA

Na MWANDISHI MAALUM
Dhana ya uwajibikaji kutokana na makosa yanayofanywa na watumishi wa umma ni nyenzo muhimu katika kudumisha utawala bora. Hata hivyo, mara nyingi dhana hiyo imekuwa ikipewa tafsiri potofu katika jamii. Sauti za kuwataka watumishi wa umma kuwajibika kwa kujiuzulu zimekuwa zikipazwa na wananchi ambao dhahiri wanaonyesha kuchukizwa na maovu, uzembe au makosa mengine makubwa yanayofanywa na viongozi wao, wakiamini kwamba wanakuwa wamepoteza sifa ya kuendelea kuwatumikia wakiwa kwenye ofisi za umma.
 Kidemokrasia,  suala la uwajibikaji husaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha nidhamu katika utumishi wa umma na kujenga maadili mema kwa viongozi hao katika utekelezaji wa majukumu yao wakitambua kwamba vyeo walivyo navyo ni ‘dhamana’.
Katika siku za karibuni kumekuwa na sauti za kumtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka awajibike kisiasa kutokana na ‘mgawo’ wa fedha anaodaiwa kupata kutoka kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta. 

Sauti hizo zilipazwa zaidi baada ya kujiuzulu hivi karibuni kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, ambaye alimuomba Rais kuachia ngazi kwa  maelezo kuwa ushauri wake kuhusiana na suala la  Akaunti ya Escrow ya Tegeta “haukueleweka na umechafua hali ya hewa.” 
Hoja inayojengwa na watu wanaomtaka Profesa Tibaijuka kuwajibika kwa kujiuzulu ni kwamba waziri huyo hakupaswa kupokea fedha kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP, Bw. James Rugemalira (hata kama zimeelekezwa kwa taasisi yake ya elimu) kwa kuwa fedha hizo zinaonekana kama hongo inayoweza kupindisha maadili yake kama waziri. 
Lakini Profesa Tibaijuka ana mtazamo tofauti kuhusu shinikizo hilo la kumtaka ajiuzulu kwa kuwa  anaamini hakutenda kosa lolote kwa kupokea fedha za mchango wa ajili ya taasisi yake ya elimu kutoka kwa Bw. Rugemalira. 

Aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi iliyopita kwamba hawezi kujiuzulu kwa kuwa akifanya hivyo hataitendea haki dhana ya uwajibikaji kisiasa (political accountability) na pia Rais, aliyemteua kwenye wadhifa huo atamshangaa.
“Sikuja hapa kujiuzulu. Nijiuzulu kwa sababu gani? Kwa sababu nimepata mchango wa shule?,” Pofesa huyo wa uchumi na Katibu Mkuu Msaidizi mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN Habitat) aliwaambia waandishi wa habari, alipokuwa akijibu swali la kwa nini asijiuzulu kutokana na kuhusika kwenye sakata la Escrow Akaunti ya Tegeta. 

  Aliongeza: “Kujiuzulu sio fasheni, lazima kuwe na sababu.”
Msimamo huu wa Prof. Tibaijuka umekuja wakati ambapo wasomi na wadadisi mbalimbali wa mambo wanahoji kuhusu mwenendo wa mchakato mzima wa kushughulikia suala la Akaunti ya Escrow ya Tegeta.  Kuna wanaoamini kwamba mchakato huo uligubikwa na hisia, visasi na jazba za kisiasa badala ya kuzingatia ukweli wa mambo.
Mwanasiasa mkongwe na waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, alikaririwa hivi karibuni akiikosoa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali  (PAC) iliyowasilishwa bungeni kwamba ilikuwa na mapungufu.

 Alisema udhaifu mkubwa katika ripoti hiyo umewafanya wananchi waamini kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow zilikuwa za umma bila kuzingatia ukweli kwamba fedha hizo zilitokana na tozo ya gharama ya uwekezaji (capacity charges) kwenye mitambo ya kufua umeme ya IPTL.
Prof. Tibaijuka, kwa upande wake, ameeleza kushangazwa kwake na hatua ya PAC kutomuita ili kumhoji kuhusu fedha alizopokea kutoka kampuni ya VIP na badala yake kumhukumu bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.
Aidha, mshangao wa Prof. Tibaijuka unatokana na ukweli kwamba hakuna sehemu yoyote katika taarifa zote za ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya Escrow ya Tegeta, pamoja na umiliki wa kampuni ya IPTL ambapo jina lake linatajwa.
Lakini pia katika taarifa yake, kufuatia matokeo ya ukaguzi maalum wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye akaunti hiyo, PAC inakiri kwamba haikuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu umiliki, uhalali au uharamu wa fedha hizo na watu waliogawiwa fedha zilizotokana na akaunti hiyo.
Udhaifu mwingine wa mchakato huo unajionyesha katika maazimio ya bunge ambayo pia waziri Tibaijuka anasimamia kujenga hoja zake; wakati ambapo Bunge limeishauri mamlaka ya uteuzi pamoja kumuwajibisha yeye na wengine wanaotajwa, katika azimio lingine bunge hilo hilo linataka vyombo husika viwachunguze watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya PAC na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi.
Ni katika hatua hii ndipo Prof. Tibaijuka anahoji iweje mamlaka ya uteuzi ishauriwe kumuwajibisha wakati suala hilo halimuhusu na hana dhamana nalo? Anasema jambo hilo linakiuka kanuni za misingi ya haki ya asili ambayo ni kutomhukumu mtu yeyote wakati uchunguzi wa jambo ukiendelea na bila kumsikiliza. 

Nakubaliana na Prof. Tibaikuja katika hoja hii anaposema hiyo “sio dalili ya kuheshimu msingi  wa utawala bora wa utoaji haki.”
Hata hivyo, waziri huyo ambaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa hakwenda kwenye mkutano huo kutetea madhambi, amesema atakuwa tayari kurejesha fedha zilizotolewa na VIP iwapo itathibitishwa kwamba fedha hizo ni haramu.  Alisisitiza kuwa iwapo kuna madhambi yanapaswa kushughulikiwa.
Lakini kwa sasa, Prof. Tibaijuka anasema anaona fahari kuchangiwa fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya elimu ya wasichana ambayo amekuwa akiipigania kwa miaka mingi kama mwanaharakati wa maendeleo.
Hii ilikuwa fursa nzuri kwa waziri huyo wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi kuelezea upande wake baada ya kunyimwa fursa hiyo bungeni. “PAC ilinishangaza, ingawa nilikuwa Dodoma hawakuniita. Ningeitwa ningeyasema haya ninayowaeleza hapa,” aliwaambia waandishi wa habari.    Anasema madhara yanayotokana na maamuzi yasiyozingatia ukweli yanaweza kuwa makubwa kwa taifa.

No comments: