Tangazo

December 18, 2014

Watanzania wengi hawana uelewa kuhusu tatizo la usonji - Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda – Maelezo

Watanzania wengi hawana uelewa  wa tatizo la usonji (Autism)  kwa watoto hivyo basi uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa jamii unahitajika  ili watu watambue  tatizo hilo na kuweza kuwasaidia watoto hao.

Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma kikwete wakati akiongea na Prof. Andy Shih ambaye ni Makamu wa Rais Mwandamizi wa Mambo ya kisayansi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Autism Speaks katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizopo jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alisema  jamii ikiwa na uelewa kuhusu watoto hao kutakuwa na mabadiliko kwa wazazi na walezi hivyo basi ni jukumu la jamii nzima kuungana na kuweza kuwasaidia watoto hao ili waweze kupata elimu na mafunzo maalum.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alimpongeza Prof. Shih kwa kazi anayoifanya ya kuwasaidia watoto wenye usonji Duniani na kwa kitendo chake cha kuamua kuwasaidia watoto wa Tanzania.

Kwa upande wake Prof. Shih alisema tatizo la usonji linatibika kama watoto watapewa mafunzo mapema na  jamii ikipata elimu na kulifahamu tatizo hilo itaweza kuwasaidia watu wenye matatizo hayo kupata huduma.

Alisema alitembelea shule ya msingi Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha kutoa huduma ya watoto wenye usonji na kujionea hali halisi na kuahidi kushirikiana na wadau wengine ili waweze kutatua changamoto zilizopo.

Taasisi ya WAMA kwa kushirikiana na wadau wa Afya nchini na Taasisi ya kimataifa ya Autism Speaks  yenye makao yake mjini New York Marekani  watafanya kazi kwa pamoja  ili kutumia vitendea kazi na utaalam wao ambao wameukusanya kwa miaka mingi kuwasaidia watoto wenye matatizo ya usonji nchini.

Kazi watakazozifanya ni pamoja na  kuunda timu ndogo ya wataalam wa mitaala na mafunzo ambao watapitisha miongozo na mitaala iliyopo pamoja na ile ya Autism Speaks na kupendekeza utaratibu wa mafunzo ya makundi mbalimbali wakiwemo watoa huduma.

Timu hiyo inaandaa utaratibu wa mafunzo ya wazazi, walezi na familia ya mtoto mwenye matatizo ya usonji, kuandaa mwongozo unaokubalika wa kuwapima na kuwatambua watoto wenye usonji, kuandaa mitaala na miongozo ya ufundishaji wa watoto wenye usonji na kutumia jukwaa na program za kitaifa kuwalinda watoto.

Wakati wa Mkutano wa  69 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UN) uliofanyika mwishoni mwa mwezi wa tisa mwaka huu mjini NewYork Marekani Mama Kikwete alikutana na Prof. Shih ambaye aliahidi kufanya kazi na WAMA ili kuwasaidia watoto wenye tatizo la usonji ambao wataweza kupata elimu na huduma ya afya kama watoto wengine.

No comments: