Tangazo

January 8, 2015

AG Masaju: Watumishi wa Umma tufanye kazi kwa uzalendo



Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju (kushoto) akibadilishana mawazo na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro Jumatano, Januari 7, 2015, wakati alipofika Wizarani kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais jakaya Kikwete hivi karibuni.
XXXXXXXXXXXXX

Na Mwandishi Wetu

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju amewakumbusha watumishi wa umma katika sekta ya sheria kufanya kazi kwa ushirikiano na uzalendo ili kulinda maslahi ya taifa.

Bw. Masaju, ambaye ameteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo, amefafanua kuwa watumishi wa umma wanapozingatia uzalendo katika utendaji wao, wanapata nguvu ya kusimama na kukemea maovu.

Bw. Masaju ameyasema hayo leo (Jumatano, Januari 7, 2015) jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria alipokwenda kubadilishana nao mawazo.    

“Sisi kama Wizara kwa ujumla wetu, tunapaswa kuwa mfano wa uzalendo katika taifa hili ili tunaposimama mbele ya watu, tuwe na nguvu kwa kuwa tupo safi,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro alimpongeza Bw. Masaju kwa heshima aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete na kuahidi kuwa yeye na Wizara itaendelea kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.

“Tunakupongeza kwa heshima kubwa uliyopewa na Mheshimiwa Rais na sisi kama wasimamizi wa sera, tutaendelea kutoa ushirikiano kwako kama tulivyofanya kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyetangulia,” alisema Waziri Migiro.

Aidha, Waziri Migiro aliahidi kuongeza ushirikiano katika kuimarisha kada ya Mawakili wa Serikali pamoja na watumishi wengine ili kuongeza ufanisi katika utoaji haki.

Bw. Masaju aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 2 Januari mwaka huu na kuapishwa tarehe 5 Januari. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Aidha, Bw. Masaju amewahi kuwa Mshauri wa Sheria wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments: