Tangazo

January 23, 2015

Serikali za Marekani na Ujerumani kushirikiana na Serikali ya Tanzania na Frankfurt Zoological Society ili kuokoa Tembo katika hifadhi ya Selous

Waziri Nyalandu akibalidilishana hati na Balozi wa Ujerumani Tanzania  Egon Kochanke, baada ya kutiliana saini mkataba wa ujerumani kuipa Tanzania msaada wa vifaa vya kisasa vya kukabiliana na majangili katika mbuga ya wanyama ya Selous.
XXXXXXXXXXXXX

 
HIFADHI YA SELOUS, TANZANIA.  Katika jitihada za kukabiliana na tatizo kubwa la ujangili katika hifadhi ya wanyamapori ya Selous, serikali za Marekani na Ujerumani zimekabidhi vifaa mbalimbali vitakavyotumiwa na askari wanyamapori wanaofanya doria katika hifadhi hiyo. 

Makabidhiano hayo yalifanyika Jumatano iliyopita katika Hifadhi ya Selous. 

Vifaa vilivyokabhiwa ni pamoja na mahema madogo na makubwa, tochi, ramani, darubini, kamera, sare na viatu. 

Mbali na msaada huo, serikali ya Ujerumani ilitangaza ahadi ya kusaidia uboreshwaji wa baadhi ya miundombinu ya hifadhi ikiwa ni pamoja na barabara, viwanja vya ndege na makazi kwa askari wa wanyamapori. 

Kwa upande wake, serikali ya Marekani itatoa wakufunzi kutoka katika Jeshi la Marekani watakaotoa mafunzo kwa askari wa wanyama pori kuhusu mbinu za doria na matunzo ya magari.
Hafla hii iliyohudhuriwa na Balozi wa Marekani, Mark Childress na Balozi wa Ujerumani Egon Kochanke wakiwa na mwenyeji wao Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Lazaro Nyalandu,  ililenga sio tu katika makabidhiano ya vifaa  bali pia katika kusisitizia umuhimu wa ushirikiano na uratibu wa pamoja wa jitihada za kukabiliana na ujangili miongoni mwa mataifa mbalimbali, kati ya sekta ya umma na sekta binafsi na ndani ya serikali ya Tanzania yenyewe. 
Msaada huu wa vifaa na mafunzo  kutoka Marekani ni sehemu ya programu yake ya kukabiliana na ujangili na kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori nchini kote Tanzania itakayogharimu Dola za Kimarekani milioni 40 katika kipindi cha miaka minne ijayo. Nayo, programu ya serikali ya Ujerumani ya kukabiliana na ujangili na kuimarisha uhifadhi nchini Tanzania itagharimu Dola za Kimarekani milioni 51 itakapokamilika hapo mwaka 2016,  hii inajumuisha kiasi cha Dola milioni 21 zilizotengwa kwa ajili ya hifadhi ya Selous. 
  Katika hafla hii mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na uhifadhi wanyamapori yaliwakilishwa na Bw. Gerald Bigurube Meneja wa programu ya  taasisi ya Frankfurt Zoological Society nchini Tanzania.

No comments: