Meneja Mkuu wa Royal Valentino
Hotel iliyopo Kariakoo Dar es Salaam, Kapara Hamis (kushoto) akizungumza na
waandishi wa habari jana kuhusiana na semina ya waandishi chipukizi wa habari
za michezo inayoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA), itakayofanyika Jumatano ijayo. Kulia ni Mkurugenzi wa Redio Times FM,
Rehure Nyaulawa ambaye redio yake pamoja na hoteli hiyo ndiyo wadhamini wa
semina hiyo. Mwingine ni Makamu Mwenyekiti wa TASWA, Egbert Mkoko. (Na
Mpigapicha Maalum).
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Mwandishi Wetu
REDIO Times FM ya Dar es Salaam
imejitokeza kuwa mdhamini mkuu wa semina ya waandishi wa habari za michezo
chipukizi itakayafanyika Jumatano wiki ijayo.
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi
wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Egbert Mkoko alimkshukuru Mkurugenzi
Mkuu wa Redio Times FM, Rehure Nyaulawa na Meneja wa Valentino Royal Hotel,
Kapara Hamis kwa kukubali kugharamia semina hiyo ya siku moja.
“Naomba nitamke kuwa Redio Times FM
ndiyo wadhamini wa semina yetu ya siku moja itakayoshirikisha waandishi wa
habari za michezo chipukizi, ambapo Valentino Royal Hotel pia ya Dar es Salaam
watakuwa wadhamini washiriki wa semina yetu, ambayo itafanyikia hotelini kwao,”
alisema Mkoko.
Aliwashukuru wadhamini hao kwa moyo
wa kujitolea na kuiomba pia hoteli hiyo iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam
kuendelea kuipa ushirikiano TASWA na wanamichezo kwa ujumla katika masuala
mbalimbali ya udhamini.
Mkoko alisema siku zote chama chake
kimekuwa kikipigania kuandaa mafunzo kwa wanahabari wa michezo kama sehemu
mojawapo ya kukuza weledi na kwamba wana matumaini Aprili watafanya nyingine
kama hiyo na pia Mei mwaka huu watafanya nyingine.
Alisema wataalamu wa michezo
mbalimbali kama vile soka, riadha, netiboli, kikapu watapata fursa ya kutoa
mada kuhusiana na michezo yao, ambapo pia waandishi wa habari za michezo
waliobobea wameitwa kuwaweka sawa chipukizihao, ambao wameteuliwa kutokana na
mapendekezo ya wahariri wa habari za michezo wa vyombo husika.
“Hii ni awamu ya kwanza kwa
waandishi wachanga na baadhi ya wa kada ya kati ambao jumla yao ni 40, baada ya
hapo tutaendesha mafunzo ya namna hii kwa waandishi waandamizi na wahariri wa
habari za michezo.
“Tunaamini baada ya hapo kutakuwa
na mabadiliko ya namna fulani, kwani watu tuliowaandaa nina hakika washiriki
watashiba vizuri,” alisema na kuongeza kuwa pia kutakuwa na mtoa mada kutoka
Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM).
Kwa upande wake Nyaulawa alisema
redio yake ikiwa ni mdau mkubwa wa habari na michezo kwa ujumla amekuwa
akipigania mafunzo kwa wanahabari wa michezo kama sehemu mojawapo ya kukuza
weledi.
“Tunaamini waandishi wanapoboresha
uandishi wao inachangia kwa kiasi kikubwa kukuza heshima ya vombo vya habari,
hivyo tunaomba wadau mbalimbali washirikiane na TASWA inapoandaa mambo kama
haya, sisi tumeanza na wengine wasaidie,” alisema.
Naye Kapara wa Valentino Royal,
alisema hoteli yake imekuwa ikitumiwa pia na timu mbalimbali zinapotoka nje ya
nchi kufikia hapo, hivyo kwa namna ya pekee waandishi wa habari za michezo ni
wadau wao, ndiyo sababu hawakusita kukubali kudhamini mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment