Tangazo

March 23, 2015

Wafanyakazi wa Airtel wadhamini ujenzi wa darasa la shule ya watoto wa mahitaji maalum - Pongwe Tanga



Wafanyakazi wa Airtel Tanzania wakiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma kwa  Jamii, Bi. Adriana Lyamba (wa pili kushoto), kubeba mabati kwa ajili ya kupaua darasa litakalotumiwa na wanafunzi wenye ulemavu katika Shule ya Msingi Pongwe jijini Tanga hivi karibuni.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Mwandishi Wetu, Tanga

WAFANYAKAZI wa Airtel wadhamini ujenzi wa darasa la shule ya watoto wa mahitaji maalumu Pongwe Tanga.

Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imesaidia ujenzi wa darasa kwa ajili ya watoto wenye ulemavu katika shule ya msingi Pongwe iliyopo nje kidogo ya Jiji la Tanga.

Darasa hilo limejengwa ikiwa ni jitihada za kampuni hiyo kusaidia maendeleo ya elimu nchini kupitia mpango wa “Tunakujali” unaohusisha wafanyakazi wake kuchangia katika shughuli za kijamii.

Mkurugenzi wa Huduma za jamii wa kampuni ya Airtel Bi Adriana Lyamba amefanya ukaguzi wa ujenzi huo na kuahidi kuendelea kusaidia mpango wa elimu kwa makundi yenye mahitaji muhimu hapa nchini. 

Bi Lyamba amesema kuwa msaada huo umetokana na mahitaji ya miundombinu kwa jamii ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwenye shule hiyo ambayo kwa Jiji la Tanga ndiyo inatoa elimu kwa watu wenye ulemavu.

“Sisi Airtel tumeona umuhimu wa wanafunzi wenye ulemavu na tumetambua mahitaji yao ndio maana tumekuja na mpango huu wa ujenzi wa Darasa hapa Pongwe” alisema Bi Lyamba.

“Ujenzi wa Darasa hili ni sehemu ya mpango wetu wa kusaidia ukuaji wa elimu hapa nchini kupitia kampeni yetu ya shule yetu na tunaamini utasaidia makundi yote ya jamii” aliongeza Bi Lyamba. 

Mwalimu mkuu Msaidizi wa shule hiyo Bw. Mfaume Kamba amesema, msaada huo wa ujenzi wa chumba hicho utasaidia sana kupunguza tatizo la wanafunzi wenye mahitaji maalumu kukosa sehemu ya kujifunzi.

Bw. Mfaume amesema, Jengo hilo ni msaada mkubwa kwa wanafunzi wa awali kwenye shule hiyo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisomea nje kutokana na kutokuwepo kwa chumba cha kusomea.

“Msaada huu ni mkombozi kwetu kwani kwa sasa wanafunzi wetu wa awali watakuwa na mahala pazuri kwa kusomea na kuondokana na adha ya kujifunza wakiwa kwenye mazingira ya nje” alisema Bw. Mfaume.

Shule hiyo ya Mchanganyiko ya msingi ya Pongwe bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vyumba vya kutosha vya kujifunzi kwa watu wenye ulemavu na vifaa vyake.

No comments: