Tangazo

April 16, 2015

UNDP YAZITAKA REDIO JAMII KUONGEZA HAMASA WATU KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA

Na Mwandishi wetu

SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini limetoa wito kwa redio za jamii kujikita zaidi katika kutoa hamasa ya ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi ukiwamo kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Akizungumza matumaini ya Umoja huo katika tathmini ya mradi wa Uwezeshaji wa Demokrasia (DEP) kwa Redio za Kijamii nchini Tanzania zinazounda umoja wa COMNETA, chini ya ufadhili wa UNESCO, mtaalamu wa masuala ya mawasiliano wa UNDP Nicodemus Marcus alisema kwamba redio hizo zina kazi 5 muhimu kuelekea uchaguzi.

Alisema pamoja na kutekeleza makubaliano kati ya Umoja wa Mataifa na redio hizo kuhusu elimu kuelekea uchaguzi mkuu unaozingatia maadili ya uandishi na uwajibikaji katika mradi huo ni matumaini ya UNDP kwamba redio hizo zitatimiza wajibu wa kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika kwa amani na makundi mbalimbali yanajitokeza kupitia vyama vyao vya kisiasa kuwania uongozi.

Akifafanua alisema kwamba hamasa ya watu kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, kushiriki katika kura ya maoni,Kujitokeza kwa wingi katika upigaji kura, kuendeleza amani kuelekea katika uchaguzi mkuu na kuhamaisha makundi kuwania uongozi ni mambo matano ambayo Umoja wa Mataifa unategemea redio hizo zitafanya.
Aidha alisisitiza haja ya redio hizo kufuata makubaliano ya kuendesha elimu kwa uadilifu mkubwa ili wasijiingize katika matatizo yoyote yale yatakayokwamisha kazi ya kutoa elimu kwa umma kuelekea uchaguzi mkuu na mchakato wake.

Naye Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu ambaye taasisi yake ndiyo inayosimamia redio za jamii alisema kwamba Tathmini ya mradi wa uwezeshaji wa demokrasia (DEP) kwa radio za kijamii, umeonesha kuwapo kwa changamoto hasa katika utekelezaji wa makubaliano.

Alisema kati ya redio 28 zilizomo katika umoja wa Comneta ni redio kama 8 zilizofanya juu ya kiwango na kuonesha kwamba inawezekana kuhabarisha umma.

Ufanisi wa redio hizo umeoneshwa katika ripoti ya Umoja wa Vilabu vya waandishi wa UTPC uliopewa kazi ya kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya mwaka jana kuhusu uendeshaji wa vipindi mbalimbali vya uchaguzi katika mradi wa DEP.

Alisema redio zilizofanya vyema ni pamoja na Mpanda iliyopata alama 80 huku redio nyingine za Fadeco FM , Fadhila FM, Sibuka FM, Mazingira FM, Kwizera FM Kyela FM na Micheweni zikiwa na alama 60.

Pamoja na changamoto hiyo Bi. Rose Haji Mwalimu alisema wamejifunza kwamba kumekuwepo na kuboreka kwa vipindi kiasi ya kwamba watu wengi wanavutiwa kusikiliza redio hizo na wengine wakitaka kufanyanao kazi.
DSC_0392
Mtaalamu wa mawasiliano Mradi wa uwezeshaji wa demokrasia (DEP) kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Nicodemus Marcus akizungumza wakati wa kufunga warsha ya siku tatu ya kutathmini mradi wa uwezeshaji wa demokrasia na amani (DEP) kwa wanamtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA) yenye lengo la kuimarisha ushiriki wa redio za jamii nchini kuelekea uchaguzi 2015 na kura ya maoni iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Huria Tanzania jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wa pili kushoto ni Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu,akifuatiwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Prof. Tolly Mbwete, Mwenyekiti wa mtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Jamii ya Wilayani Karagwe ya FADECO FM, Bw.Joseph Sekiku na Mshauri wa UNESCO, Balozi mstaafu Mh. Christopher Liundi.

Aidha wametambua kwamba redio za jamii ndio mhimili mkubwa wa kupata taarifa mbalimbali za uchaguzi zilizofanyiwa kazi hasa uwapo wa watoa habari wa kuaminika katika jamii.

Pia alisema redio hizo zimeanza kuona umuhimu wa kufuata maadili, ushirikishaji kijinsia, utoaji wa nafasi kwa makundi mbalimbali wakiwemo walemavu na vijana katika kazi.

Hata hivyo alisema kwamba mapungufu yaliyojitokeza yalisababishwa na viongozi wa redio kupuuzia suala la uwajibikaji na pia kuwakoesha vitendea kazi watumishi husika na umbali wa maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi kutoka katika ofisi zilizopo redio husika.

Viongozi pia katika tathmini walishauriwa kuwapa motisha watendaji wao kwani walionekana kulalamikia suala la kukosa motisha katika kazi ambazo wanastahili kuzifanya ili kufuata maelekezo ya mradi wa DEP.

Wakati huo huo Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (THRDC) moja ya taasisi inayotetea usalama wa waandishi wa habari maeneo ya kazi imewataka washiriki katika warsha wasipofuata maadili hawataweza kufanyakazi zao vyema ikiwa ni pamoja na kuingia katika migogoro na wadau wa habari.

Naye Balozi Christopher Liundi mshauri wa UNESCO amesisitiza pia haja ya kufuata maadili na pia kuhakikisha redio za jamii zinajijenga kupitia mtandao wao na kujiuza kwa umma.

Aidha alishauri kwamba ripoti ya UTPC igawiwe kwa wadau wote kwani imetengeneza msingi wa utendaji kazi katika radio za jamii ambazo kwa sasa zinakuja kasi katika kuhabarisha mambo mbalimbali kwa jamii hasa vijijini.

Katika tathmini hiyo ya mradi wa DEP walikuwepo wawakilishi kutoka Ofisi ya Msajili, Tume ya taifa ya uchaguzi (baba nay a Visiwani), Under the same Sun, Human Rights Defenders Coalition(THRDC) na taasisi nyingine zinazogusa masuala ya uchaguzi na amani.
DSC_0158
Mhariri wa Redio Kwizera FM ya Ngara mkoani Kagera, Seif Omary Upupu akichangia mada wakati wa warsha ya siku tatu ya kutathmini mradi wa uwezeshaji wa demokrasia na amani (DEP) kwa wanamtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA).
DSC_0166
Mhariri wa Sibuka FM, Anita Balingilaki akishiriki kuchangia mada kwenye warshi hiyo.
DSC_0289
Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu akifafanua jambo kwa washiriki wa warsha hiyo.
DSC_0020
Pichani juu na chini ni baadhi ya Wanamtandao wa redio jamii 28 nchini (COMNETA) waliohudhuria warsha hiyo ya siku tatu ya kutathmini mradi wa uwezeshaji wa demokrasia na amani (DEP) kwa wanamtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA) yenye lengo la kuimarisha ushiriki wa redio za jamii nchini kuelekea uchaguzi 2015 na kura ya maoni iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
DSC_0018 DSC_0288
Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu akizungumza na wanamtandao wa redio jamii nchini (COMNETA) waliohuhduria warsha ya siku tatu ya kutathmini mradi wa uwezeshaji wa demokrasia na amani (DEP) iliyomalizika mwishoni mwa juma lililopita katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Makamu mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Meneja wa Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Telecentre Sengerema FM, mkoani Mwanza Bw. Felician Ncheye pamoja na Mwenyekiti wa Gender and Media in Southern, Tanzania Chapter (GEMSAT) Dominica Haule.
DSC_0284
Mratibu wa Mradi wa uwezeshaji wa Demokrasia na Amani (DEP) kutoka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bi. Beatrice Stephano akizungumzia ushiriki wao na majukumu kwenye mradi wa DEP kwa wana-COMNETA.
DSC_0028
Makamu mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Meneja wa Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Telecentre Sengerema FM, mkoani Mwanza Bw. Felician Ncheye (kulia) akiwa na wadau kutoka Under the Same Sun walioshiriki kutoa mada kwenye warsha hiyo.

No comments: