Tangazo

May 15, 2015

MATANGAZO YA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA YAREJESHWA TENA



Na  Magreth Kinabo- MAELEZO

Baraza la  Tiba asili na Tiba mbadala limerejesha  utoaji wa  matangazo yanayohusu  huduma  hizo, lakini  kwa kufuata  Sheria,ambayo inataka yawe yamepitiwa na baraza hilo.

Hayo yalisemwa leo na Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wa Mikoa na Wilaya, Mboni  Bakari wakati akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu urejeshaji wa matangazo hayo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR), jijini Dares  Salaam. 

 Alisema  matangazo yanayohusu huduma hiyo   sasa yameruhusiwa   kwa mujibu wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala  Namba 23 ya mwaka 2002,ambapo kipengele namba 15 kifungu cha kwanza cha sheria hiyo kinataka matangazo hayo  yawe yamepelekwa katika baraza hilo ili liweze kuyapitia  na kuangalia  kama yapo sahihi.

“Baraza  kama chombo tunayo haki ya kusimamia  , tuko hapa kwa ajili ya kusimamia afya ya Watanzania. Hivyo matangazo yanapaswa kutolewa chini ya sheria hii na baraza linatoa kibali . Baraza limekataza kutoa matangazo bila ya kufuata sheria,” alisema  Bi. Mboni.

 Naye Kaimu Mkurugenzi wa huduma hizo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Paulo Mhame alisema  watoaji wa huduma hizo wanapaswa kuhakikisha dawa zao  lazima  zimefanyiwa utafiti   kabla ya kuzitangaza.

 Alisema iwapo  mtumiaji atatumia dawa na hakupona   anaweza  kuwasilisha malalamiko yake katika baraza hilo  na pia    katika sheria hiyo kipengele namba 4 kinamruhusu mtumiaji  kumpeleka mtoa huduma  mahakamani. 

Baraza hilo lilisitisha utoaji wa matangazo hayo Agosti 28, mwaka 2014 na kurejesha rasmi tangu Machi 16,mwaka 2015.   

No comments: