Tangazo

August 25, 2015

Washindi Airtel Rising Stars Dar watunukiwa

 Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi, Boniface Wambura akimkabidhi Kombe nahodha wa timu ya Harmburg Queens Jamila Kassim baada ya kuwa mabingwa katika michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mkoa wa kisoka wa Ilala. Hafla ya kukabidhi kombe ilifanyika jana katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Jijini Dar-es-Salaam.
Wachezaji wa timu ya Mchanganyiko FC wakishangilia baada ya kuwa mabingwa katika michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mkoa wa kisoka wa Kinondoni. Hafla ya kukabidhi kombe ilifanyika jana katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Jijini
Dar-es-Salaam.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Michuano ya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Aitel Rising Stars kwa mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke jana ilifungwa
rasmi katika uwanja wa Karume ambapo mabingwa wa mikoa husika walikabidhiwa zawadi zao.


Kwa upande wa wasichana, Hamburg Queens walifanikiwa kutawazwa mabingwa wa mkoa wa Ilala huku Bombom wakitwaa taji la ubingwa wa mkoa huo kwa upande wa wavulana.


Katika mkoa wa Temeke upande wa wasichana, timu ya Evergreen ndio walitangazwa mabingwa na Wakati Ujao ndio walioibuka wababe kwa upande wa wavulana katika mkoa huo.


Kwa mkoa wa Kinondoni, timu ya wasichana ya Mburahati Queens walifanikiwa kuwa mabingwa wakati Mchanganyiko FC wakitangazwa
mabingwa kwa upande wa wavulana.


Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Jackson Mmbando, alitoa shukrani zake za dhati kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) pamoja na vyama vya mikoa kwa ushirikiano wao ambao unawapa nguvu ya kuendelea kudhamini programu hiyo ya soka kwa vijana.


“Mwaka huu tumeshuhudia uboreshaji mkubwa zaidi wa mashindano haya baada ya ujio wa timu za wasichana ambao wameongeza msisimko wa michuano hii. Pia naamini tutapata wavijana wenye vipaji ambao watasaidia kutangaza taifa letu hapo baadaye katika ngazi za
kimataifa”, alisema Mmbando.


“Shukrani zangu nazipeleke pia kwa Makatibu wa mikoa shiriki kwa kufanikisha kupata vijana bora na wenye weledi ambao ni nuru ya taifa
letu kwa siku za usoni”, aliongeza.


Kwa upande wake mgeni rasmi, Boniface Wambura ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, alisema anaipongeza Airtel kwa mchango wao hapa nchini wa kuvumbua vipaji vya vijana ambao ni manufaa kwa taifa kwa siku za baadaye.


“Nimefarijika kuona vijana wakijituma na kucheza kwa ari kubwa licha ya umri wao mdogo, jambo ambalo litawafikisha mbali katika maisha yao ya soka, kitu cha msingi ni kuhakikisha hamkati tama ili kuweza kufikia malengo” alisema Wambura.


“Sisi TFF, tutahakikisha michuamo yote inayohushisha vijana inaendeshwa kwa weledi wa hali ya juu ili kupata vijana bora watakaoweza kulisaidia taifa letu kuanzia timu za vijana mpaka za wakubwa hapo baadaye”, Wambura aliongeza.

Wakati huo huo mikoa hiyo mitatu ya kisoka jana imeanza kutoana josha katika mashindano ya Airtel Rising Stars yenye lengo la kupata
mabingwa wa mkoa wa Dar es Salaam chini ya Chama cha Mpira wa soka mkoani wa Dar es Salaam (DRFA).


Katika michezo miwili iliyochezwa jana timu ya Ilala Girls iliibuka na ushindi mnono wa magoli 4-1 dhidi ya Temeke Girls wakati timu ya
wavulana, Ilala Boys walipepetana na Temeke Boys ambapo Ilala Boys waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.Mashindano ya Airtel Rising Stars ambayo mwaka huu yanashirikisha mikoa ya Ilala, Kinondoni, Temeke, Morogoro, Mbeya, Mwanza na Arusha inatarajiwa kuingia kwenye hatu nyeti ya fainali za Taifa iliyopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, kuanzia Septamba 11 hadi 21.

No comments: