Tangazo

February 10, 2016

TFF yaipongeza SHIWATA kwa kumpatia eneo Samatta

Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Michael Kagondela (kulia) akimuonesha Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi eneo ambalo mchezaji bora wa Afrika, Mbwana Samatta atapimiwa ekari tano na kukabidhiwa na mtandao huo kwa ajili ya kujenga chuo cha wanamichezo, Mkuranga mkoani Pwani. Picha na Mpiga picha Wetu.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

MKURUGENZI wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi ameupongeza uongozi wa Mtandao wa wasanii Tanzania (SHIWATA)kumpatia uanachama wa heshima na kumzawadia ekari tano za eneo la ardhi mchezaji bora wa Afrika, Mbwana Samatta ili ajenge kituo cha kuendeleza michezo nchini.

Akizungumza na Katibu Mkuu wa SHIWATA, Michael Kagondela katika kijiji cha Wasanii Mwanzega, Mkuranga juzi, Madadi ambaye pia ni mwanachama wa SHIWATA alisema huo ni motisha mzuri utakaowavutia wachezaji wengine kujibidiisha kuiga nyayo za Samatta.

Alisema Samatta amefungua njia kwa wachezaji wengine ambao kuanzia sasa watajitahidi kuonesha vipaji vyao binafsi ambavyo matokeo yake vinageuka kuwa lulu katika sura ya Afrika na dunia.

Naye Katibu Mkuu wa SHIWATA, Kagondela alisema mtandao huo unaomiliki ekari 300 kwa ajili ya kujenga makazi na viwanja vya burudani na kumbi za starehe inatarajia kupata wawekezaji kuwekeza katika fani mbalimbali za michezo.

Alisema kutoka Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anna Wambura alipotembelea kijiji cha wasanii Mkuranga hivi karibuni ahadi zake za kuwapatia huduma za jamii za umeme, barabara na maji zimekuw2a kichocheo kwa wasanii kujenga nyumba zao kwa kasi.

Mwenyekiti wa SHIWATA,Cassim Taalib alisema wameanza kutekeleza rai ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga aliyoitoa hivi karibuni akiwataka SHIWATA kuandaa tamasha kubwa mwaka huu litakalowakutanisha wasanii wa fani zote nchini.

No comments: