Tangazo

April 6, 2016

fastjet yasitisha safari Kilimanjaro-Nairobi


Dar es Salaam,

Fastjet Tanzania imesitisha safari zake kati ya Kilimanjaro na Nairobi.

Fastjet ilikuwa  ikifanya safari kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwenda Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Nairobi mara mbili kwa wiki siku za Ijumaa na Jumapaili.

Kusitishwa kwa safari kwenye njia hiyo kunatokana na kuwepo mahitaji haba ya abiria kwenye masoko yote mawili ya Kilimanjaro na Nairobi hali iliyosababisha kutokuwa na manufaa kibiashara.

Shirika hilo limeeleza kuwa  lengo lake ni kuhakikisha linarudisha safari hizo kati ya Kilimanjaro- Nairobi pindi tu na wakati ambapo wateja wataihitaji.

Safari za fastjet  kutoka Dar es salaam na Kilimanjaro kwenda Nairobi zilianza Januari 11, 2016.

 Mahitaji ya abiria  kwa safari hizo  ambazo kwa kiwango kikubwa ni za kibiashara kati ya majiji  ya Dar es Salaam na Nairobi  ambayo kwa pamoja  yana idadi ya watu ambao ni zaidi ya milioni nane  yamekuwa makubwa na kuifanya fastjet hivi karibuni kuongeza safari zake  kwenye njia  hiyo  ili kukidhi mahitaji makubwa ya abiria.

Fastjet  kwa hivi sasa inafanya safari mbili za kwenda na kurudi kati ya miji hiyo  kila siku ndani ya wiki  na hivyo kufanya  jumla ya safari zake kwa wiki kati ya Uwanja wa Kimataifa wa Dar es Salaam na Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta  kuwa ni 28.

 Mtiririko mpya wa safari unawapatia wateja huduma sahihi mapema nyakati za asubuhi na  jioni  na matokeo ya ratiba hiyo  ni kuwepo kwa takribani  viti 19,000 kila mwezi kwenye safari hizo kati ya majiji hayo mawili na hali kadhalika kuwapatia wateja  mbadala sahihi wa kusafiri kwa nauli wanayoimudu.

 Nauli za fastjet kimsingi ni za chini ikilinganishwa na tozo za mashirika mengine ambayo kwa sasa yanafanya safari zake kati ya Kenya na Tanzania.

Nauli  kutoka Tanzania kwenda Kenya  zinaanzia shilingi 176,000 kwa safari moja, bila kodi ambayo ni shilingi 107,800 kwa kuondokea Tanzania  na dola 40 kwa kuondokea Kenya, na hivyo fastjet kuwashauri abiria kukata tiketi zao mapema kabla ya siku ya kuanza safari ili kutumia fursa hiyo ili kufaidi na nauli ya chini.

 Nauli kutoka Kenya zinaanzia dola za Marekani 120 kwa safari moja zikijumuishwa kodi za serikali ambayo ni dola 40 kwa kuondokea Kenya.

Matokeo ya safari hizi kati ya Nairobi na Dar es Salaam yamekuwa ni makubwa kutokana na ukweli unaojidhihirisha kwamba nauli kwenye mashirika shindani yanayofanya safari kati ya nchi hizi mbili zimeshuka kwa kiwango cha asilimia 40 tangu fastjet ianzishe safari zake.

Fastjet inasisitiza kwamba  kupunguza mtiririko wa safari kwenye njia kati ya Nairobi na Kilimanjaro kunafungua fursa  ya kuongeza uwezo zaidi kwa njia zilizopo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na hali kadhalika kuwepo uwezekano wa kufungua njia nyingine mpya siku za karibuni. 

No comments: