Baadhi ya wasanii wa Tanzania waliowahi kushiriki Coke Studio.
Imetangaza pia muziki wa Bongo Fleva
Onyesho maarufu la muziki la Coke Studio Africa, ambalo hivi sasa limeingia katika awamu ya tano chini ya udhamini wa kampuni ya Coca-Cola, limechangia kwa kiasi kikubwa kutangaza wasanii wa Tanzania waliofanikiwa kushiriki na kazi zao nje ya nchi hususani wanaopiga muziki wa Bongo Flava.
Kazi za wasanii zimejulikana kutokana na mtindo unaotumika katika onyesho hili la kuwakutanisha wasanii nguli kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambapo hufanya kolabo za pamoja ambazo zinarushwa kupitia vituo vya luninga na kufuatiliwa na wapenzi wengi wa muziki kupitia mitandao ya kijamii.
Baadhi ya wasanii kutoka Tanzania ambao wameshiriki onyesho hili tangu lianzishwe ni Lady Jaydee, Diamond Platnumz, Vanessa Mdee, Alikiba, Joh Makini, Shaa, Fid Q, Ben Pol, John Makini, Shaa, Nahreel na msimu huu wa tano wapo Rayvanny, Izzo Bizness na Nandy.
Misimu minne iliyopita ya Coke Studio Africa imekuwa na mafanikio makubwa katika kuutangaza muziki wa Bongo Flava barani Afrika.
Wamejiongezea mashabiki, wamejifunza mambo mbalimbali kuhusu muziki kama burudani, muziki kama taaluma na muziki kama biashara na tena si tu kutoka kwa wasanii wenzao wa Afrika na Marekani pia.
Vilevile wasanii wote ambao wamepita kwenye onyesho hili wameendelea kupata mafanikio makubwa ya kimuziki kutokana na kazi zao kuendelea kutamba na kukubalika kwa wengi ndani na nje ya Tanzania.
Taarifa kutoka kampuni ya Coca-Cola iliyotolewa hivi karibuni imeeleza kuwa onyesho la Coke Studio Africa, ambalo umaarufu wake umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka msimu huu utakuwa na burudani za aina yake kutoka kolabo za wasanii nguli barani Afrika kuanzia Afrika Magharibi mpaka Afrika ya Kusini na litarushwa na vituo vya luninga kwenye nchi zaidi ya 30 barani Afrika.
Tangia onyesho hili lianzishwe limekuwa kiungo kikubwa cha kuwakutanisha wanamuziki wa Afrika kufanya kazi kwa pamoja na kupiga muziki wenye vionjo kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ikiwemo kuleta burudani kubwa kwa washabiki wa muziki wa kiafrika na kuwaunganisha waafrika hususani vijana kupitia muziki.
Katika msimu wa Coke Studio Africa unaotarajia kuanza kurushwa kwenye luninga mapema mwezi ujao unashirikisha wasanii kutoka katika nchi za Kenya, Afrika ya Kusini, Uganda, Tanzania, Rwanda, Ethiopia, Nigeria, Ghana, Angola, Zimbabwe, Togo, Cote d’Ivoire, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, DRC na Cameroon.
No comments:
Post a Comment