Tangazo

August 14, 2017

“IKUNGI ELIMU CUP 2017” KUANZA KURINDIMA JUMAMOSI AGOSTI 19 WILAYANI IKUNGI

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu
Na Mathias Canal, Singida

Kivumbi cha Mashindano ya ligi ya mpira wa miguu Wilayani Ikungi Mkoani Singida Maarufu kama “IKUNGI ELIMU CUP 2017” kinataraji kuanza kurindima Wilayani Ikungi Siku ya Jumamosi Agosti 19 huku mashindano hayo yakiwa na dhamira ya kuwafikia zaidi ya wananchi 5000 katika Wilaya hiyo.

Mashindano hayo yatakayofunguliwa na Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Dkt Rehema Nchimbi na kuzikutanisha timu mbalimbali kutoka Kata zote 28 na vijiji 101 katika Wilaya ya Ikungi huku yakiongozwa na kauli mbiu ya “ Changia, Boresha Elimu Ikungi”.

Ufunguzi wa mashindano hayo utafanyika siku ya Jumamosi kuanzia saa tano asubuhi katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Ikungi ambapo mechi ya ufunguzi itakuwa ni kati ya timu ya Kata ya Ikungi na Timu ya Kata ya Puma ambapo kabla ya kufunguliwa kwa mashindano hayo kutakuwa na mchezo dhidi ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida waatakaovaana vikali na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Katika mchezo huo wa awali Timu ya Madiwani kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ikungi itaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji J. Mtaturu huku timu ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe Elias Tarimo.

Katika ufunguzi wa mashindano hayo kutakuwa na zoezi la uanzishwaji rasmi wa zoezi la ufyatuaji matofali kila Kata ambapo zaidi ya matofali 300,000 yanahitajika ikiwa ni sehemu ya kuhimiza utatuzi wa Changamoto mbalimbali Wilayani Ikungi ikiwemo Upungufu wa nyumba za walimu, Vyumba vya madarasa, Ofisi za walimu, Maabara, Thamani mbalimbali, Matundu ya vyoo vya walimu na wanafunzi.

Akizungumza na mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu alisema kuwa katika ufunguzi wa mashindano hayo pia kutakuwa na zoezi la kukabidhi zawadi kwa shule ya sekondari Ikungi iliyofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita na kupelekea kuongoza kikanda kwa wanafunzi 16 kupata Daraja la kwanza.

Alisema kuwa aliwapa motisha wanafunzi kwa kuwaahidi kumpatia shilingi 100,000 kwa kila mwanafunzi atakayefanya vizuri katika matokeo yake hivyo utekelezwaji wa ahadi hiyo utafanyika siku ya ufunguzi wa mashindano hayo.
 
Aidha, zawadi zingine zitakazotolewa itakuwa ni kuwapa kila mwalimu takribani shilingi milioni moja kwa ajili ya kuakisi ufanisi wao kwa kuwafundisha wanafunzi kwa weledi mkubwa na hatimaye kuwa na matokeo mazuri.

Kuanza kwa mashindano hayo ya “IKUNGI ELIMU CUP 2017” ni utekelezaji wa Wazo la kuanzisha Mfuko wa Elimu lilitokana na kikao cha wadau wa elimu kilichoitishwa na Mkuu huyo wa Wilaya mwezi Disemba, 2016 na kubaini changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwemo kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi mpaka Sekondari.

Katika Kikao hicho kuliadhimiwa maazimio 43 ambayo yalizaa wazo la kuanzisha mfuko wa elimu ambapo wazo hilo lilifikishwa kwenye baraza la madiwani na kupokelewa kwa kauli moja ndipo mwezi Aprili mwaka 2017 baraza liliridhia kuanzishwa mfuko na kuteua wajumbe 15 wa bodi ya mfuko wa elimu wa Wilaya ya Ikungi.

Jumla ya fedha taslimu shilingi bilioni 3 zinahitajika kwa mpango mkakati wa miaka mitatu kwa mtazamo wa Shule zenye hali mbaya zaidi ambapo wadau wanaombwa kuchangia mfuko ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi  kuchangia 3% ya mapato yake ya ndani.

No comments: