Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein akizungumza Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Mtukufu Sheikh Saud
Bin Saqr Al Qasimi na kufanya nae mazungumzo yaliolenga kuendeleza uhusiano na
ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.
Mazungumzo hayo yaliofanyika katika makaazi ya Sheikh Saud Bin
Saqr Al Qasimi mjini Ras-Al-Khaimah, ambapo viongozi hao kwa pamoja walieleza
haja ya kuendeleza uhusiano na kuimarisha mashirikiano katika kuinua sekta za
maendeleo ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia.
Aidha, viongozi hao walizungumza juu ya hatua zinazoendelea katika suala
zima la utafiti wa mafuta na gesi asilia ambapo katika mazungumzo hayo
walieleza haja ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pamoja ili kufikia lengo la
kuipaisha Zanzibar kiuchumi na kimaendeleo.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alitoa shukrani kwa kiongozi huyo kutokana
na juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kumpongeza kiongozi huyo
kwa mafanikio yaliopatikana nchini humo katika kipindi kifupi.
Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar ina mengi ya
kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ras Al Khaimah na iko tayari kupanua wigo wa
maendeleo kutoka nchini humo kwani inatambua mafanikio yaliopatikana kutokana
na mikakati iliyowekwa.
Pamoja na hayo, viongozi hao kwa pamoja walizungumzia hatua zaidi
zinazohitajika katika kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Ras Al Khaimah
katika sekta za maendeleo ikiwa ni pamoja na kupanga mipango madhubuti katika
malengo yaliokusudiwa ya hapo baadae.
Nae Kiongozi huyo alieleza kuwa Ras Al Khaimah itaendeleza uhusiano na
ushirikiano wake na Zanzibar hasa katika sekta hizo za maendeleo na kusisitiza
kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaletea maendeleo makubwa Zanzibar hasa kwa
kutambua kuwa jambo hilo limo kwenye dhati ya moyo wake.
Alieleza kuwa uhusiano
na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo una malengo ya kuhakikisha wananchi wa
Zanzibar wanapata maendeleo endelevu huku akizipongeza juhudi na kasi za Rais
Dk. Shein za kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua za kiuchumi.
Katika maelezo yake
Mtawala wa Ras Al Khaimah alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa atandelea
kumuunga mkono ili kuhakikisha malengo yaliokusudiwa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kupambana na umasikini na kukuza uchumi yanatekelezeka kwa
vitendo kwani kuna kila dalili za kuyatekeleza kutokana na juhudi anazoziona ambazo
zinafanywa na Dk. Shein pamoja na Serikali anayoiongoza.
Wakati huo huo, Dk. Shein
alikutana na uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta
na Gesi Asilia ya Ras Al Khaimah “Rak
Gas”, iliyopo mjini Ras Al Khaimah ambapo katika maelezo ya uongozi wa Kampuni
hiyo walimueleza Dk. Shein hatua zilizofikiwa za utafiti wa mafuta na gesi
asilia Zanzibar.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu
wa Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Kamal
Ataya alimpongeza Dk. Shein kwa ziara yake hiyo na kuahidi kuendeleza
ushirikiano uliopo huku akisisitiza kuwa Kampuni yake itahakikisha utafiti
unaofanyika unakuja na majibu mazuri.
Dk. Shein kwa upande
wake alitoa pongezi zake kwa Mtawala wa Ras Al Khaimah pamoja na kuipongeza
Kampuni hiyo kwa jitihada zake inazochukua katika kuhakikisha malengo
yaliokusudiwa yanafikiwa na hatimae kuleta tija.
Mapema, Rais Dk. Shein
akiwa na ujumbe wake akiwemo Mama Mwanamwema Shein, walitembelea eneo la
Kisiwa cha Al Marjan ambacho kimetengezwa baada ya kufukiwa kwa bahari na kuwa
mji wa kisasa wa kitalii na uwekezaji.
Akiwa katika eneo hilo,
Dk. Shein alipata maelezo juu ya hatua zilizochukuliwa katika kulitengeneza
eneo hilo la bahari na sasa kuwa ardhi iliyojengwa hoteli za kisasa ambazo
zimekuwa ni kivutio kikubwa cha watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Aidha, uongozi wa Kisiwa
hicho ulimueleza Rais Dk. Shein hatua zilizochukuliwa katika kuhakikisha hata
watalii wakiwemo wananchi wa Ras Al Khaimah wanapata fursa ya kutalii katika
eneo hilo kwa kuweka viwango vya chini vya malipo ya hoteli hizo ili kuhakikisha wenye vipato vya chini nao
wanafaidika.
Dk. Shein akiwa nchini
Dubai pia, alipata fursa ya kukutana na ujumbe wa Utaratibu wa Mfuko
unaojulikana kwa jina la “Khalifa Fund” ambapo uongozi wa Mfuko huo ulimueleza
Rais Dk. Shein namna unavyotoa fursa zake na kuahidi kutoa ushirikiano kwa
Zanzibar hasa katika mpango wa kuwawezesha vijana kujikomboa na ajira na
kuahidi miongoni mwa nchi zitakazowapa kipaumbele Zanzibar itakuwa ni ya mwanzo.
Rais Dk. Shein amemaliza
ziara yake ya wiki moja katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na anatarajiwa
kurejea nchini kesho Jumamosi,
tarehe 27 Januari, 2018.
Ziara hiyo ya Dk. Shein ilianza
kwa kufanya mazungumzo na Mtukufu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi
wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya
(UAE) nchini Abu Dhabi ambapo pia,alifanya mazungumzo na Mohamed Saif Suwaid, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko
wa Maendeleo ya Abudhabi “Abudhabi Fund for Development”, na kutembelea mji wa
Nishati, Masdar, msikiti wa Shaikh Zayed pamoja na sehemu ya kihistoria ya
Wahat Al Karama.
Aidha, Dk. Shein alifanya
ziara nchini Dubai kufanya mazungumzo na Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al
Makhtoum, Makamo wa Rais na Waziri Mkuu wa (UAE) na Mtawala wa Dubai, alitembelea
Bandari ya Jebel Ali, alikutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wenyeviwanda
wa Dubai na kutembelea Mji mpya wa kisasa wa Nakheel pamoja na Mradi wa Palm
Jumeirah.
Dk. Shein alifanya ziara
mjini Sharjah na kukutana pamoja na kufanya mazungumzo na Mtukufu Dk. Shaikh
Sultan Mohammed Al Qasimi, Mtawala wa Sharjah,akiwa Sharjah, alitembelea eneo
la shughuli za uvuvi la ‘East Fishing Processing LLC” pamoja na shamba la
ngombe wa maziwa la Al Rawabi.
Pia, Dk. Shein alifanya
ziara Ras Al Khaimah na kukutana pamoja na kufanya mazungumzo na Mtukufu Shaikh
Saud Saqr Al Qasimi, Mtawala wa Ras Al Khaimah pamoja na kutembelea Makao Makuu
ya Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na gesi asilia ya Ras Al Khaimah “Rak Gas” pamoja na
kutembelea kisiwa cha Al Marjan.
Katika
ziara hiyo, Dk. Shein alifuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mkewe Mama
Mwanamwema Shein, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud
Talib, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohamed, Waziri Asiyekuwa
na Wizara Maalum Juma Ali Khatib,pamoja na Mshauri wa Rais Masuala ya
Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
Wengine
ni Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Juma Ali Juma, Balozi
Mohamed Haji Hamza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki kwa upande wa Zanzibar, Mkurugenzi Mtendaji wa
Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum Khamis Nassor pamoja na watendaji wengine
wa Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
No comments:
Post a Comment