Na Hamza Temba - Dodoma
..........................................................
Serikali imeanza utekelezaji wa mkakati wa kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini unaohusisha upanuzi wa maeneo ya kijeografia yenye vivutio pamoja na mazao ya utalii ili sekta hiyo ichangie zaidi kwenye pato la taifa na kuondoa umaskini katika jamii.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma.
Alisema kwa upande wa mkakati wa kupanua jeografia ya vivutio vya utalii nchini Serikali itafungua utalii wa ukanda wa kusini kwa kuboresha vivutio na miundombinu ambapo tayari imesaini mkataba wa mkopo nafuu kutoka benki ya dunia wa milioni 150 za kimarekani sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 340 za kitanzania kwa ajili ya mradi wa REGROW ambao utasimamia maliasili na kuendeleza utalii wa ukanda wa kusini.
Alisema kupitia mradi huo jumla ya viwanja vya ndege 15 vitaboreshwa ndani ya Pori la Akiba la Selous na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na uwanja wa ndege wa Nduli uliopo mjini Iringa. Maeneo mengine yatakayoboreshwa katika hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo ni Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na Mikumi.
"Mradi huo utaboresha pia usafiri wa reli kwa kuimarisha kituo cha Matambwe ambacho ni kitovu cha utalii katika Pori la Akiba la Selous",. Alisema Dk. Kigwangalla.
Akizungumzia upanuzi wa mazao ya utalii, alisema sekta hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea zaidi utalii wa wanyamapori huku ukiegemea zaidi katika ukanda wa kaskazini kwa zaidi ya asilimia 90.
Alisema kwa sasa Serikali itapanua wigo wa mazao hayo ya utalii ambapo mwezi Septemba kila mwaka utakuwa mwezi maalum wa maadhimisho ya urithi wa Tanzania (Urithi Festival) kwa ajili kuimarisha utalii wa kiutamaduni na kuhamasisha utalii wa ndani.
Alisema Serikali kupitia Wizara yake itaimarisha pia utalii wa fukwe na utalii wa mikutano.
Awali Dk. Kigwangalla alisema sekta ya Utalii ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa ambapo huchangia asilimia 17.6 ya pato la taifa, asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni na asilimia 12 ya ajira zote nchini.
Alisema pamoja na mafanikio hayo sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi na kuegemea zaidi kwenye vivutio vya ukanda wa kaskazini huku vivutio vya kanda nyingine vikiwa havichangii ipasavyo kwenye pato la taifa.
No comments:
Post a Comment