Tangazo

April 20, 2018

SERIKALI YAANZISHA MPANGO WA KUTOA MAFUNZO KWA VIJANAKUKIDHI MAHITAJI YA VIWANDA VYA NGUO


Mhe. Charles J. Mwijage (Mb), Waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, akizungumza wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018. Picha Zote Na Mathias Canal, NFRA
Baadhi ya wakuu wa mikoa inoyozalisha Pamba kwa wingi wakifatilia mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.
Mgeni-Rasmi Waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, Mhe. Charles J. Mwijage (Mb), akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.
Naibu waziri wa Kilimo, Mhe. Dkt Mary Mwanjelwa akijadiliana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Antony Mtaka wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.
Waziri wa kilimo, Mhe. Dkt Charles Tizebawakati akifatilia kwa makini mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.
Baadhi ya  wadau wa sekta ya pamba wakifatilia kwa makini mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.

Na Mathias Canal, Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na viwanda vya nguo na mavazi imeanzisha mpango maalum wa kutoa mafunzo ya ushonaji kwa vijana kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda vya nguo.

Upatikanaji wa ujuzi wa aina hiyo utapunguza gharama kwa wawekezaji na kuongeza ufanisi katika uzalishaji. Vilevile, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia msaada wa Gatsby Africa, kimeendelea kutoa mafunzo ya Shahada ya Teknolojia ya Nguo (Textile Degree) ambapo, mwaka 2016/2017, Chuo kilitoa wahitimu 44 ikilinganishwa na wahitimu 13 kwa mwaka 2015/2016. Lengo ni kuhakikisha kuwa kuna wataalam wa kutosha wa fani ya ubunifu na uzalishaji mavazi nchini.

Hayo yamebainishwa na Mhe. Charles J. Mwijage (Mb), Waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018
Alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazozalisha pamba kwa kiasi kikubwa barani Afrika, ikiwa na zaidi ya wakulima 500,000 wanaolima pamba katika eneo linalokadiriwa kufikia hekta 412,000 katika mikoa 13 nchini. Sekta ya nguo na mavazi ni moja ya sekta za Kipaumbele katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini na inahusisha mnyororo mrefu wa uongezaji thamani kuanzia kuchambua pamba (ginneries); kusokota nyuzi (spinning); kuseketa vitambaa (weaving); kufuma vitambaa (knitting), kuchapa na kutia rangi (processing) na kushona mavazi (garments).
Aliongezaa kuwa Sekta hii ni moja ya sekta muhimu katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuanzisha viwanda vinavyoajiri watu wengi kwa wakati mmoja. Sekta hii itawezesha kupunguza uingizaji wa nguo kutoka nje na kuongeza matumizi ya pamba inayolimwa nchini pamoja na malighafi nyingine zinazopatikana nchini kama vile magadi na gesi asilia.
Hata hivyo, Serikali imeendelea kuzishawishi taasisi za Umma kwa kuanzia majeshi na hospitali ili wanunue nguo na mavazi yanayozalishwa na viwanda vya ndani.  Lengo ni kuhakikisha kuwa utaratibu wa makusudi unawekwa kwa Taasisi za umma kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu hapa nchini. Kwa mfano uvaaji wa fulana aina ya Polo Shirt kwa wafanyakazi wote katika siku moja ya wiki, na pia wanafunzi wote shule za msingi na sekondari kuvaa sare hizo. Inakadiriwa kuwa kuna jumla ya wanafunzi milioni 15 na wafanyakazi wa sekta zote za umma wanafika 25,000.
Mhe Mwijage alisema kuwa Utengenezaji wa fulana moja ya polo unakadiriwa kutumia wastani wa gramu 300 za pamba, sketi moja inakadiriwa kutumia gramu 600 za pamba, kaptula moja inakadiriwa kutumia gramu 600 za pamba. Hivyo jumla ya gramu 900 za pamba zitahitajika kutengeneza sare kwa mwanafunzi mmoja awe wa kike au wa kiume.
Kama ikikadiriwa kila mwanafunzi atavaa wastani wa sare (sketi & shati au kaptula na shati) mbili tu kwa mwaka gramu 1800 (sawa na kilo 1.8) za pamba zitahitajika kwa mwanafunzi mmoja, hivyo wastani wa kilo 27,000,000 (sawa na tani 27,000) zitahitajika kwa mwaka. Endapo mahitaji yaliyokusudiwa yakipitishwa tunategemea kwamba viwanda vya ndani vitakuwa na uwezo wa kutumia asilimia 17 ya pamba yote inayozalishwa nchini kwa mwaka. Hii itahamasisha uzalishaji wa pamba, kuongeza ajira na kuongeza kipato.
Serikali inakamilisha taratibu za kuidhinisha ‘’ Blue Print’’   ambayo imeainisha maeneo ya kufanyia maboresho ya Kisera na Kisheria ili kuhamasisha uwekezaji katika Sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo sekta ya pamba nguo na mavazi” Alikaririwa Mhe Mwijage

Pia,aliwashukuru Wadau wa sekta ndogo ya pamba, nguo na Mavazi kwa kazi kubwa wanayofanya katika uzalishaji, biashara na wadau wengine kwa michango yao katika kuendeleza sekta hii. 

Mkutano huo umehusisha Wizari ya Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara wa Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo; Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge za Viwanda, Biashara na Mazingira; Bajeti; Kilimo, Mifugo na Maji; na Uwekezaji Mitaji ya Umma, Wakuu wa Mikoa; Makatibu Wakuu, Wawakilishi wa Sekta Binafsi, Maafisa wa Serikali na Taasisi za Serikali.

No comments: