Tangazo

October 27, 2011

Kampuni ya Anglo-Gold Ashanti kuilipa Serikali Kodi ya Mapato sh. bilioni 86 (sawa na dola za Marekani milioni 50) mwaka huu.

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia Baraza la Biashara la Jumuia ya Madola huko Perth Australia.

SERA sahihi za Serikali za kuyataka makampuni ya madini nchini kuanza kulipa kodi ya mapato zimeanza kuzaa matunda baada ya Kampuni ya Anglo-Gold Ashanti kutangaza kuwa italipa kodi ya sh bilioni 86 (sawa na dola za Marekani milioni 50) mwaka huu.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Bwana Mark Cutifani amemwambia Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa kati ya fedha hizo, tayari kampuni hiyo imelipa kiasi cha sh bilioni 8.6.

Bw. Cufitani amemwambia Rais Kikwete kuwa kampuni hiyo inayomiliki machimbo ya dhahabu ya Geita Gold Mine, italipa kiasi kilichobakia cha kodi hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Bw. Cutifani ameyasema hayo leo, Alhamisi, Oktoba 27, 2011, wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete kwenye Hoteli ya Holiday Inn, iliyoko kwenye Kituo cha Mikutano cha Burswood, mjini Perth, Australia ambako viongozi hao wawili wanahudhuria mikutano mbalimbali ikiwa sehemu ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuia ya Madola unaotarajiwa kuanza rasmi kesho, Ijumaa, Oktoba 28, 2011 na unaofanyika nchini Australia kwa mara ya tatu.

Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni ya Anglo-Gold Ashanti kulipa kodi ya
mapato kutokana na mapato yake tokea kuingia katika soko la Tanzania mwaka 1999, na hatua hiyo inatokana na sear ya Serikali ya kuyataka makampuni ya madini nchini kuanza kulipa kodi ya mapato baada ya kurudisha fedha zake za uwekezaji katika uchimbaji wa madini nchini.

Wakati wa mkutano huo, Bw. Cutifani pia amemwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake imeamua  kuboresha mahusiano yake na jamii ya wananchi wanaoishi karibu na machimbo hayo kwa kuongeza huduma za kijamii ambazo kampuni hiyo inatoa kwa wananchi hao.

Amesema kuwa moja ya miradi ya kijamii ambayo kampuni hiyo imeikamilisha ni ule wa maji ambao Bw. Cutifani amemwomba Rais Kikwete kuuzindua rasmi wakati atakapopata nafasi.

Mbali na Bw. Cutifani, Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na
Bwana Andrew Forrest, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Madini ya Fortsque Metal Group, yenye shughuli za uchimbaji madini katika Australia. Katika mkutano huo, Bw. Forrest ameonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika uchumi wa Tanzania katika maeneo ya uchimbaji madini na kwenye miradi ya miundombinu ya barabara na reli.

Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Bwana John Borshoff wa Kampuni ya Paladin Energy Generation ya Australia ambaye ameeleza nia yake ya kutaka kuwekeza katika uchumbaji wa madini ya uranium katika Tanzania.

Bw. Borshoff amemweleza Mheshimiwa Rais Kikwete kuwa tayari kampuni yake
inachimba madini ya uranium katika nchi za Malawi na Nambia na ingependa
kuingia katika shughuli hiyo nchini Tanzania.

Imetolewa na:
 Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini Perth, Australia.

No comments: